Marekani kuendelea kupambana na al-Qaeda hadi kuimaliza
3 Mei 2011Mshauri wa ngazi ya juu wa ikulu ya Marekani anayehusika na mapambano dhidi ya ugaidi , amesema leo kuwa nchi hiyo ina lenga kuuharibu kabisa uongozi wa juu wa kundi la kigaidi la al-Qaeda, hivi sasa ambapo kiongozi wake Osama bin Laden ameuawa na uwezo wa kundi hilo kuharibiwa kutokana na operesheni za majeshi ya Marekani. Tangu mashambulio ya mwaka 2001 dhidi ya miji ya New York na Washington , kundi la al-Qaeda limeeneza mtandao wa makundi shirika katika mashariki ya kati na Afrika ya kaskazini na kutoa hamasa kwa mashambulizi yanayofanywa na makundi ya watu wanaojulikana kama wapiganaji waliozaliwa na kukulia katika mataifa ya Ulaya na Marekani.
Mkuu wa kitengo kinachopambana na ugaidi katika ikulu ya Marekani John Brennan amesema kuwa kifo cha Osama bin Laden ni moja kati ya mfululizo wa operesheni za Marekani ambazo zimeleta kipigo kikubwa kwa uongozi wa juu wa kundi la al-Qaeda nchini Pakistan na Afghanistan katika muda wa miaka ya hivi karibuni.
Tutajaribu kuchukua nafasi hii tuliyonayo hivi sasa kwa kifo cha kiongozi mkuu wa al-Qaeda, kuhakikisha kuwa tunna uwezo wa kuharibu kabisa kundi hilo, amesema Brennan. Tuna nia ya kufanya hivyo na tunaamini tunaweza.
Tunaamini kuwa tumeliharibu kundi hili, kupunguza uwezo wake na kufanya kuwa vigumu kwa kundi hili kufanyakazi zake ndani ya Pakistan na hata nje ya mipaka ya nchi hiyo.
Mwenyekiti wa kamati ya uhusiano wa kimataifa ya baraza la seneti la Marekani John Kerry amesema kuwa mashambulio ya Marekani ya ndege zisizokuwa na rubani dhidi ya maeneo ya makabila nchini Pakistan yameuwa zaidi ya viongozi wa ngazi ya juu wa al-Qaeda 17 kabla ya kifo cha bin Laden.
Mkurugenzi wa CIA Leon Panetta ameonya jana kuwa kifo cha Bin Laden kinaweza kuwafanya waungaji wake mkono kujaribu kufanya aina fulani ya kulipiza kisasi. Waziri mkuu wa zamani wa Uingereza Tony Blair amesema kuwa nadharia ya bin Laden bado iko hai.
Mapambano bado hayajakwisha. Nadharia ambayo bin Laden anaiwakilisha, kwamba Uislamu umo katika mapambano na mataifa ya magharibi , na kwamba Uislamu umo vitani na sisi, nadharia hii bado iko hai. Bado wako watu wanafikiria hivyo, bado inafanyakazi duniani, na tunapaswa kuendelea hadi pale tutakapoweza kuishinda na kuiondoa.
Marekani huenda ikatoa baadaye leo picha za Osama bin Laden wakati akizikwa baharini lakini uamuzi wa mwisho bado haujafanywa, amesema afisa wa Marekani leo.
Kwa upande mwingine kuuwawa kwa Osama bin Laden nchini Pakistan ni kitu kinachoinua morali wa majeshi ya kimataifa yanayopigana nchini Afghanistan, lakini haitafanya chochote muhimu kufuta kabisa mapigano yanayoendeshwa na kundi la Taliban wanasema wachambuzi wa mambo.
Wakati huo huo polisi wa Uingereza wamewakamata watu watano chini ya sheria ya kupambana na ugaidi karibu na kinu cha kinuklia , lakini wamesema kuwa tukio hilo halionekani kuhusika na kifo cha mkuu huyo wa kundi la al-Qaeda Osama bin Laden.
Mwandishi : Sekione Kitojo / afpe/rtre
Mhariri : Mohammed Abdul-Rahman