1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Marekani kuipa Ukraine mfumo wa Patriot, Urusi yatoa onyo

15 Desemba 2022

Urusi imeiita mipango ya Marekani ya kuipatia Ukraine mifumo ya kujilinda na makombora aina ya Patriot kuwa ni uchokozi na hatua ya kujiimarisha kijeshi kwenye mzozo kati yake na Ukraine.

Abschuss-Manöver Patriot-Raketenabwehr
Picha: IMAGO

Urusi inaikosoa hatua ya Marekani ya kuipatia Ukraine mifumo hiyo ya kujilinda, huku majirani hao wakiondoa kabisa uwezekano wa kusitisha mapigano katika kipindi cha sikukuu za Christmas na mwaka mpya. 

Msemaji wa wizara ya mambo ya kigeni wa Urusi Maria Zakharova amesema leo kwamba silaha zote zinazopelekwa na mataifa ya magharibi nchini Ukraine zinaonyesha namna yanavyohalalisha kuvilenga vikosi vya Urusi. Amesema hayo katika taarifa yake ya kila wiki.

"Tungependa kuwakumbusha watu kwamba silaha zote zinapelekwa na mataifa ya Magharibi nchini Ukraine ni shabaha halali dhidi ya majeshi ya Urusi na huenda zikakamatwa ama kuharibiwa. Tayari tumekwishasema mara kadhaa," alisema Zakharova.

Soma Zaidi:Rais Zelensky aomba msaada zaidi G7

Picha ikionyesha mfumo wa kujilinda wa Marekani ambao unaandaliwa kupelekwa nchini Ukraine.Picha: JACK GUEZ/AFP/Getty Images

Washington inakamilisha mipango yake ya kupeleka mfumo huo wa kujilinda na makombora wa Patriot nchini Ukraine ambayo inatarajiwa kutangazwa wiki hii, hii ikiwa ni kulingana na maafisa watatu waipozungumza na shirika la habari la Reuters siku ya Jumanne. Mfumo huo unatajwa kuwa ni wa kisasa zaidi miongoni mwa mifumo ya kujilinda ya Marekani.

Ubalozi wa Urusi mjini Washington umesema mkakati huo ni uchokozi unaoweza kusababisha matokeo ambayo hayakutarajiwa.

Wakati hayo yakijiri, vikosi vya Ukraine mapema leo vikifanya mashambulizi makali zaidi ya makombora mashariki ya nchi hiyo ambako kunadhibitiwa na Urusi. Maafisa waliowekwa na Moscow wamesema, wakati pande zote mbili zikisema hakuna makubaliano ya kusimamisha mapigano wakati wa Christmas. Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema suala hilo la kusitishwa kwa mapigano si sehemu ya ajenda. Ikumbukwe vita hivi vimedumu kwa takriban miezi 10 sasa.

Soma Zaidi:Urusi yazidisha mashambulizi ya angani Ukraine Mashariki

Kwa upande wa Ukraine, Jenerali Oleksiy Gromov pia amepangua uwezekano huo wa kusitisha mapigano katika kipindi chote cha sikukuu, akimaanisha Christmas na mwaka mpya, alipozungumza na waandishi wa habari mapema leo. Akasisitiza kwamba hakutakuwepo na mapigano iwapo tu hakutakuwepo na mvamizi wa aina yoyote kwenye ardhi yao.

Kumeshuhudiwa uharibifu mkubwa wa makazi katika maeneo mengi nchini Ukraine kutokana na mashambulizi ya UrusiPicha: Artur Widak/AA/picture alliance

Moscow na Kyiv kwa sasa hawajihusishi na mazungumzo ya aina yoyote ya kuumaliza mzozo huo mkubwa kabisa kushuhudiwa Barani Ulaya tangu enzi ya Vita vya Pili vya Dunia, na ambao umeshika makali zaidi katika eneo la mashariki na kusini mwa Ukraine.

Raia wa Ukraine wanateseka kwa baridi, huku rais akiomba Umoja wa Mataifa kuiadhibu Urusi

Taarifa zinasema watu wawili wameuawa kufuatia mashambulizi yalioyofanywa na Urusi katika mji wa Kherson kusini mwa Ukraine, hii ikiwa ni kulingana na ofisi ya rais, likiwa ni shambulizi la karibuni zaidi tangu Ukraine ilipourejesha mwezi uliopita baada ya awali kuchukuliwa na Urusi.

Katika hatua nyingine, Mkuu wa shirika la haki za binaadamu la Umoja wa Mataifa Volker Turk ameliambia Baraza la Usalama la Umoja huo kwamba mamia ya raia waliuawa wiki chache baada ya Urusi kuivamia Ukraine, hali aliyoifananisha na uhalifu wa kivita.

Amesema ofisi yake imerekodi visa 441 vya mauaji ya moja kwa moja na watu kunyongwa katika mikoa mitatu tu ya Ukraine kati ya Februari 24 hadi Aprili 6 na kuongeza kuwa huenda idadi hiyo ikawa juu wakati wakifuatilia madai ya mauaji ya watu wengine 198 katika mikoa hiyo.

Ruka sehemu inayofuata Gundua zaidi
Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW