1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuishinikiza Israel kutoshambulia maeneo ya kiutu

12 Septemba 2024

Marekani imesema siku ya Alhamisi kuwa itaendelea kuishinikiza Israel kuchukua hatua zaidi ili kuepusha maafa kwenye maeneo ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.

Nuseirat I Shambulio la Israel katika jengo la makaazi Gaza
Shambulio la Israel katika jengo la makaazi GazaPicha: Omar Naaman/REUTERS

Kauli hiyo ya Marekani imetolewa na Waziri wake wa mambo ya nje Antony Blinken siku moja baada ya shambulio la anga la Israel kwenye shule ya Umoja wa Mataifa ilikuwa ikiwapokea wakimbizi wa ndani wa Kipalestina huko Nuseirat ambalo lilisababisha vifo vya Wapalestina 18.

Shule hiyo inayofahamika kama al-Jawni, ilikuwa ikimilikiwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la kuwahudumia wakimbizi wa Kipalestina UNRWA na kwamba sasa Marekani inalenga kuishinikiza Israel kuyaepusha na mashambulizi maeneo yanayofahamika kama ya kibinaadamu.

Soma pia: Watu 40 wauawa katika kambi ya al-Mawasi huko Gaza

Mamlaka za Palestina zimesema kuwa mashambulizi ya Israel katika maeneo mbalimbali huko Gaza yamesababisha vifo vya watu 34 leo Alhamisi wakiwemo wanawake 19 na watoto kadhaa.

WHO: Maelfu ya watu wamejeruhiwa Gaza

Wapalestina wakiwatafuta manusura baada ya shambulizi la Israel huko RafahPicha: Khaled Omar/Xinhua/picture alliance

Shirika la Afya Duniani WHO limesema kuwa jumla ya watu 22,500 waliojeruhiwa kutokana na vita vya Gaza wanahitaji matibabu ya muda mrefu na kwamba baadhi yao watahitaji miaka kadhaa ili kurejea katika hali zao za kawaida.

Kulingana na utafiti wa WHO yenye makao yake mjini Geneva-Uswisi, bado kuna mahitaji makubwa ya matibabu iwe ya kisaikolojia ama wagonjwa wanaohitaji kuwekewa viungo bandia pamoja na vifaa vya kuwasaida wagonjwa kutembea.

Soma pia: WHO yaomba msaada wa haraka wa vifaa tiba katika Ukanda wa Gaza

Mwakilishi wa WHO huko Gaza Rik Peeperkorn amesema wanahitaji msaada wa haraka katika eneo hilo na kwamba hawawezi kusubiri zaidi huku akitoa wito wa kuwepo usitishaji vita na mpango wa kudumu wa amani. Aidha Peeperkorn amesema:

" Tunahitaji haraka iwezekanavyo kurejeshwa kwa njia salama kwa watu wanaohitaji matibabu maalum kutoka Gaza hadi Jerusalem Mashariki na Ukingo wa Magharibi. Tunahitaji njia ya kwenda Misri, Jordan na bila shaka nchi zingine ambazo ziko tayari kupokea wagonjwa kutoka Gaza. Tunakadiria kuwa zaidi ya watu 10,000 wa Gaza wanahitaji kuhamishwa kwa ajili ya matibabu, huku nusu yao wakiwa na majeraha yanayohusiana na vita na kutokana na kiwewe, na nusu nyingine wakiwa ni wale wenye magonjwa sugu."

Mwakilishi wa WHO huko Gaza Richard (Rik) Peeperkorn Picha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Aidha WHO imesema inakamilisha siku ya mwisho ya kampeni ya chanjo ya polio  na kwamba walifanikisha zoezi hilo kwa zaidi ya watoto 552,000 walio chini ya umri wa miaka 5.

Soma pia: Watu 18 wauawa kwenye kambi ya UNRWA huko Gaza

Hayo yakiarifiwa, serikali ya Uturuki mjini Ankara imetangaza kuanzisha uchunguzi wake kuhusu kifo cha mwanaharakati mwenye uraia pacha wa Uturuki na Marekani ambaye alipigwa risasi na kuuawa wiki iliyopita na wanajeshi wa Israel katika Ukingo wa Magharibi unaokaliwa kimabavu na Israel.

Umoja wa Mataifa umeonya kuwa vita vya Israel dhidi ya Hamas vimeudidimiza uchumi wa Gaza, huku hali ikiwa ni ya kutisha zaidi katika Ukingo wa Magharibi.

(APE, AFP,DPAE)