1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuiuzia Ujerumani mifumo 600 ya ulinzi ya Patriot

16 Agosti 2024

Marekani Alhamis iliidhinisha uuzaji wa mifumo karibu 600 ya kujilinda angani dhidi ya makombora aina ya Patriot, kwa Ujerumani kwa gharama ya dola milioni 5, kulingana na wizara ya ulinzi ya Marekani.

Bundeswehr in Litauen
Picha: PETRAS MALUKAS/AFP

Katika taarifa Shirika la Ulinzi la Marekani DSCA lilisema uuzaji huo utaimarisha uwezo wa Ujerumani wa kukabiliana na vitisho vya sasa na baadae na kuongeza uwezo wa kujilinda wa jeshi lake.

"Pendekezo hili litaunga mkono sera ya kigeni na kitaifa ya Marekani kwa kuimarisha usalama wa mwanachama wa Jamii ya kujihami ya NATO ambaye ni nguvu muhimu kwa ustawi wa kisiasa na kiuchumi barani Ulaya," ilisema taarifa hiyo.

"Itaunga mkono lengo la Ujerumani la kuimarisha ulinzi wake wa kitaifa na kimpaka pamoja na ushirikiano na Marekani na vikosi vya NATO."

Uuzaji huo pia utajumuisha vifaa vinavyohusiana na mifumo hiyo vikiwemo vifaa vya kupima, vya mazoezi na vifaa vya akiba na ukarabati pia.

Shirika la DSCA, Alhamis, lilisema limewasilisha nyaraka zinazohitajika ili kulifahamisha bunge la Congress kuhusiana na uwezekano huo wa mauazo hayo.

Ujerumani ilikuwa imetuma mifumo mitatu ya ulinzi wa angani ya Patriot kwa Ukraine pamoja na makombora yanayohusiana na mifumo hiyo, tangu Urusi ilipoanza uvamizi wake mnamo Februari mwaka 2022.

Mifumo ya angani ya ulinzi ya Patriot inaweza kutumika kukabiliana na ndege za kivita za adui, mizinga na makombora ya masafa marefu. Makombora ya ulinzi yanaweza kulenga shabaha kutoka umbali wa kilomita 100 na usawa wa bahari wa hadi kilomita 30.