Marekani kupunguza uchunguzi wa mawasiliano
10 Agosti 2013Akizungumza na waandishi wa habari kwenye Ikulu ya Marekani jana Ijumaa (09.08.2013), Rais Obama amesema kuwa mipango hiyo inaandaliwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba watu wa Marekani wanakuwa na imani na juhudi zinazofanywa na serikali yakiwemo mashirika ya kijasusi.
Rais Obama ameuambia ulimwengu kwamba Marekani haina nia ya kuwafuatilia watu wa kawaida.
Amesema ataliomba bunge kufanyia mageuzi moja ya ibara ya sheria ya uzalendo iliyopitishwa baada ya mashambulizi ya Septemba 11, mwaka 2001 kifungu namba 215, ambacho kinaipa serikali uwezo wa kusikiliza mawasiliano ya simu pamoja na kukusanya data nyingine za raia wake.
Amesema serikali lazima iangalie tena jinsi inavyofuatilia ulinzi wa nchi yake dhidi ya ugaidi, huku pia ikilinda uhuru wa raia wake.
Rais Obama amesema serikali yake itafanya juhudi kubwa za kuwepo uwazi, ikiwemo kuanzisha mtandao utakaokuwa unaelezea shughuli za kijasusi.
Bodi ya wataalamu wa nje kuteuliwa
Aidha, amesema kuwa ataiteua bodi ya wataalamu wa nje watakaosimamia na kufuatilia kwa karibu shughuli za kijasusi na kutoa ripoti yake ifikapo mwishoni mwa mwaka.
Alipoulizwa kuhusu Snowden, Rais Obama, amesema kuwa viongozi wa nchi hiyo wataendelea kufanya kila wawezalo ili kumfikisha mahakamani. Snowden, amepewa hifadhi nchini Urusi.
Utata umejitokeza tangu Snowden atoe hadharani siri za shirika la kijasusi la Marekani. Rais Obama aliahirisha mkutano wake na Rais wa Urusi, Vladmir Putin, kutokana na nchi hiyo kumpatia Snowden hifadhi.
Ama kwa upande wa uhusiano kati ya Marekani na Urusi, Rais Obama amesema anatathmini upya uhusiano huo, kutokana na tofauti ya masuala kadhaa yaliyopo baina ya nchi hizo.
Tofauti ya Marekani na Urusi
Amesema tukio la hivi karibuni la Snowden kupatiwa hifadhi na Urusi ni moja kati ya masuala kadhaa wanayotofautiana katika miezi kadhaa iliyopita. Amesema tofauti hizo zinajumuisha pia mzozo wa Syria, kujilinda na makombora pamoja na suala la haki za binaadamu.
Amesema ni vyema Marekani ikapata muda wa kutathmini ni wapi Urusi inaelekea, nini maslahi yao ya msingi na kuangalia tena uhusiano ili kufanya mambo mazuri kwa ajili ya Marekani na pengine kwa Urusi pia.
Wakati huo huo, maafisa wa Marekani na Urusi wamekubaliana kuhusu haja ya kuanza kwa mkutano wa amani nchini Syria mjini Geneva, mapema iwezekanavyo.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi, Sergei Lavrov amesema kuwa watakutana tena mwishoni mwa mwezi huu kuandaa mazungumzo hayo. Lavrov amesema kuwa mazungumzo hayo yaliyofanyika mjini Washington, kati ya maafisa wa kidiplomasia na ulinzi wa Marekani na Urusi, yalikuwa ya mafanikio.
Mkutano huo umefanyika siku kadhaa baada ya Urusi kuamua kumpatia hifadhi Snowden. Lavrov na mwezake wa Marekani, John Kerry wamekiri kuwepo tofauti katika masuala kadhaa wanapoelekea katika mazungumzo hayo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE,AFPE,
Mhariri: Sekione Kitojo