Marekani kusubiri kwanza suala la vikwazo kwa Iran
12 Novemba 2013Hayo yanajiri wakati Urusi ikiarifu kuwa Iran haikuwa kikwazo cha kupatikana muafaka katika mazungumzo ya hivi karibuni mjini Geneva.
Kerry anatarajiwa kuongoza serikali ya Rais Barack Obama katika juhudi za hivi karibuni kuzuia vikwazo zaidi dhidi ya Iran, huku makundi yanayoiunga mkono Israel yakiwa na wasiwasi huenda Marekani ikawa inalegeza msimamo wake kuhusu mazungumzo na Iran.
Kerry ataihutubia kamati ya bunge ya masuala ya kibenki ya Marekani, kesho Jumatano (13.11.2013), baada ya mataifa matano yenye nguvu pamoja na Ujerumani, kushindwa kufikia makubaliano na Iran katika mazungumzo ya Geneva, yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita kuhusu mpango wake wa nyuklia.
Seneta Tim Johnson, mwenyekiti wa kamati hiyo, amesema hatofanya maamuzi jinsi ya kuendelea na suala la kuiwekea vikwazo Iran hadi baada ya mkutano wao wa siri. Lakini baadhi ya wabunge muhimu tayari wameelezea msimamo wao wakitaka vikwazo vikali viwekwe kwa Iran, kutokana na mazungumzo ya Geneva.
Ikulu ya Marekani yasema hakuna haja ya vikwazo
Ikulu ya Marekani imekuwa ikisisitiza kwamba hatua kama hiyo itadhoofisha diplomasia. Vikwazo vilivyowekwa mwaka uliopita na Marekani na Umoja wa Ulaya, vinajumuisha kuzuia mafuta ya Iran kusafirishwa kwenda nje ya nchi kwa karibu mapipa milioni moja kwa siku. Vikwazo hivyo vimeisababishia Iran hasara ya mabilioni ya Dola na imeongeza mfumuko wa bei kwa Iran na ukosefu wa ajira.
Wakati huo huo Urusi imekanusha kwamba Iran inapaswa kulaumiwa kwa kushindwa kukubali kuhusu mkataba wa kihistoria wa mpango wake wa nyuklia kwenye mazungumzo ya Geneva. Urusi imesema kuwa kushindwa kwa makubaliano hayo, kumetokana na kutokuwa na umoja miongoni mwa mataifa sita yenye nguvu duniani.
Kauli hiyo inapingana na ile ya Kerry, aliyesema mataifa matano yenye kura ya turufu katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani, yaliungana kwa pamoja kwenye mazungumzo hayo na kwamba Iran ndiyo haikukubaliana na pendekezo lililotolewa.
IMF kuutathmini uchumi wa Iran
Ama kwa upande mwingine Shirika la Kimataifa la Fedha-IMF, linapanga kuutathmini uchumi wa Iran mwanzoni mwa mwaka ujao, ikiwa ni mara ya kwanza katika kipindi cha miaka miwili.
Afisa wa shirika hilo ambaye amezuru Iran, amesema kuwa ujumbe wa shirika hilo utaruhusu kutathmini vikwazo vya mataifa ya Magharibi.
Vikwazo vilivyowekwa kwa Iran kutokana na mpango wake wenye utata wa nyuklia, vimezorotesha biashara na kuizuia Iran katika mfumo wa kibenki wa IMF tangu mwaka 2011.
Katika taarifa yake baada ya kuzuru Iran jana Jumatatu, IMF imesema ilijadiliana kuhusu mfumuko wa bei, njia ya kuufufua ukuaji wa uchumi pamoja na kuelezea mipango yake kushughulikia mageuzi ya ruzuku na masuala mengine ya kimuundo.
Mwandishi: Grace Patricia Kabogo/RTRE
Mhariri: Gakuba Daniel