Marekani kutathmini uwepo wa vikosi vyake Ulaya
18 Juni 2026
Akizungumza Alhamisi katika mkutano wa Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO, mjini Brussels, Hegseth amesema matokeo ya tathmini hiyo yatakuwa ya kweli kwa kutegemea jinsi Ulaya inavyochukua jukumu la usalama wake yenyewe kwa haraka. Amebainisha kuwa baadhi ya nchi zitashindwa katika mapitio hayo, na nchi nyingine zitafaulu vizuri.
''Tulikuwa wawazi hadharani na faragha. Hatutoruhusu tena utoaji wa pesa bure. Visingizio havihesabiki tena. Michango yetu ya NATO inategemea na nchi nyingine zinavyochukua hatua na kuchangia. Hili sio suala la upande mmoja,'' alisisitiza Hegseth.
Michango ya Marekani kutegemea nchi washirika
Mkuu huyo wa Pentagon, amesema kuanzia sasa, hatua ya Marekani kulipa ada zake ili kufidia gharama za uendeshaji wa NATO, takribani dola milioni 790 kwa mwaka 2026, itategemea namna washirika wake wanavyofikia malengo yao ya matumizi. Ameongeza kuwa pale ambapo washirika wengine hawataona umuhimu wa kuwa na dharura, michango ya Marekani itapungua.
Marekani inaongeza shinikizo kabla ya mkutano wa kilele wa NATO mwezi ujao, huku ikijitahidi kuhakikisha kwamba washirika wake wanatimiza ahadi waliyoitoa mwaka uliopita ya kuongeza matumizi katika sekta ya ulinzi.
Katibu Mkuu wa NATO, Mark Rutte amesema matumizi ya Ulaya na Canada kwa mwaka 2025, yalikuwa zaidi ya dola bilioni 90 za ziada ambazo ni sawa na ongezeko la asilimia 20 ya matumizi ya ulinzi.
Aidha, Rutte amethibitisha kuwa NATO inapitia pengine mabadiliko makubwa zaidi katika historia yake. Amesema mawaziri hao wamekubaliana kufanya mageuzi makubwa katika jeshi la NATO baada ya Marekani kutangaza kupitia upya kupelekwa kwa wanajeshi wake barani Ulaya.
Rutte amesisitiza kwamba NATO inahitaji kuyageuza haraka mabilioni ya dola za uwekezaji kuwa uwezo wa kupambana ili kuimarisha msingi wake wa viwanda dhidi ya vitisho vyovyote.
NATO yakubaliana kuimarisha uwezo wake wa nyuklia
Wakati huo huo, mawaziri hao wa NATO wamekubaliana kuimarisha uwezo wao wa nyuklia, ili kufikia maslahi yake ya usalama.
Washirika wote wa NATO isipokuwa Ufaransa ni wanachama wa Kundi la Mipango ya Nyuklia la NATO, NPG, ambalo hutumika kama jukwaa la mashauriano na kufanya maamuzi kuhusu kuzuia matumizi ya silaha za nyuklia.
Taarifa ya NPG imeeleza kuwa mawaziri wa ulinzi wa NATO wametambua kwamba vikosi vya kimkakati vya nyuklia vya muungano huo vinabakia kuwa dhamana kuu ya usalama wa washirika.