1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kutoa msaada wa chanjo milioni 1 za Mpox -Afrika

24 Septemba 2024

Rais wa Marekani Joe Biden leo atatangaza msaada wa chanjo milioni 1 za mpox na takriban dola milioni 500 kwa mataifa ya Afrika kuyawezesha kukabiliana na mripuko wa ugonjwa huo.

Chanjo ya Mpox
Chanjo ya MpoxPicha: REUTERS

Rais wa Marekani Joe Biden leo atatangaza msaada wa chanjo milioni 1 za mpox na takriban dola milioni 500 kwa mataifa ya Afrika kuyawezesha kukabiliana na mripuko wa ugonjwa huo. Haya ni kwa mujibu wa afisa mmoja mwandamizi wa serikali ya Marekani.

Afisa huyo ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Biden atatoa tangazo hilo mjini New York, ambapo anahudhuria Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa na kutoa wito kwa mataifa mengine kufuata mkondo huo.

Soma: Mataifa tajiri yahodhi mamilioni ya chanjo za Mpox

Afisa huyo amesema kuwa kwasasa hakuna kampuni ya kutengeneza dawa inayohitajika kutengezea chanjo hizo barani Afrika.

Mnamo mwezi Agosti, Shirika la Afya Ulimwenguni WHO lilitangaza mpox kuwa  dharura ya afya ya umma duniani kwa mara ya pili katika kipindi cha miaka miwili, kufuatia kuzuka kwa mripuko wa virusi vya ugonjwa huo katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ambao pia ulienea katika nchi jirani na zaidi mpaka nchini India na kuzua wasiwasi.