1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kutoa ripoti kuhusu mauaji ya Jamal Khashoggi

26 Februari 2021

Mkurugenzi wa Shirika la Ujasusi la Marekani, CIA, anatarajiwa kutoa ripoti inayotazamiwa kumshutumu mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, kwa mauaji ya mwandishi wa habari, Jamal Khashoggi.

Türkei Jamal Khashoggi Bild Wand
Picha: picture-alliance/AP Photo/L. Pitarakis

Kulingana na ushahidi uliokusanywa na CIA na mashirika mengine ya kijasusi, ripoti hiyo inatarajiwa kuonesha kuwa Mohammed Bin Salman mwenyewe, ndiye aliyeamuru mauaji ya Jamal Khashoggi, muandishi habari wa Kisaudia aliyeheshimika na aliyehamia nchini Marekani. Mauaji hayo yalifanyika katika ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, Uturuki.

Jamal Khashoggi aliyekuwa uhamishoni Marekani akiandika ripoti zinazomkosoa Mohammed Salman na serikali ya Saudi Arabia, aliuwawa tarehe 2 mwezi Oktoba mwaka 2018.

Muandishi huyo aliyekuwa na umri wa miaka 59 wakati wa mauaji yake, aliambiwa na balozi wa Saudia afike katika ubalozi wa taifa hilo mjini Istanbul, ili kupata nyaraka kadhaa alizohitaji ili aweze kufunga ndoa na mpenzi wake raia wa Uturuki, Hatice Cengiz.

Kulingana na gazeti la Washington Post, mwezi mmoja baada ya mauaji hayo, CIA ilisema kwa kujiamini kuwa mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, ndiye aliyeamuru mauaji hayo.

Kulingana na gazeti hilo ambalo Khashoggi alikuwa akituma makala zake mara kwa mara, idara za ujasusi nchini Marekani zina ushahidi wa kutosha unaoshutumu moja kwa moja Mohammed bin Salman kwa mauaji hayo, yakiwemo mawasiliano ya simu yaliyofuatiliwa kati yake na kaka yake ambaye ni balozi wa Saudia nchini Marekani.

Ushahidi mwengine ni mkanda wa sauti ya mauaji ndani ya ubalozi wa Saudi Arabia mjini Istanbul, ambao ulipatikana kupitia shirika la ujasusi la Uturuki na ambao unaweka wazi kile kilichotokea siku hiyo, na kusaidia kuwatambuwa wahusika halisi na kuonesha mawasiliano baina yao na Riyadh wakati mauaji hayo yakifanyika.

Mohammed Bin Salma akana kuhusika na muaji ya Khashoggi

Mrithi wa kiti cha ufalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, Picha: picture-alliance/AP Photo/C. Owen

Hata hivyo, mrithi huyo wa kiti cha ufalme, Mohammed bin Salman, ameendelea kukanusha kuhusika na mauaji hayo hata baada ya washauri wake wa karibu kutiwa hatiani na mamlaka za sheria nchini mwake kuwa kuhusika nayo.

Katika kujaribu kuimarisha mahusiano mazuri na Saudi Arabia, rais wa zamani wa Marekani Donald Trump alikwepa kuiwasilisha ripoti hiyo hadhrani na kumtaja Mohammed Bin Salman kama mshukiwa katika mauaji ya Kashoggi.

soma zaidi:Mauaji ya Khashoggi: Uturuki yawashtaki Wasaudi 20

Kutolewa hii leo kwa ripoti hiyo ya siri ya idara ya kijasusi nchini Marekani kumekuja wakati Rais mpya, Joe Biden, akijaribu kurejesha mahusiano ya Marekani katika eneo la Mashariki ya Kati na kurejesha kanuni za haki za binaadamu katika kiwango kinachostahili katika sera  za Marekani.

Kabla ya kutolewa kwa ripoti hiyo, Biden alizungumza kwa njia ya simu na Mfalme Salman, yakiwa mazungumzo yao ya kwanza tangu aapishwe rasmi kuwa rais wa Marekani wiki tano zilizopita.

Taarifa ya Ikulu ya Marekani haikutaja lolote kuhusu ripoti hiyo, lakini Biden siku ya Jumatano wiki hii alisema aliipokea na kuisoma.

Chanzo: afp

     

   

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW