Marekani kutoondoa vikwazo dhidi ya Sudan
10 Julai 2005Khartoum:
Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani, Robert Zoellick, amesema kuwa serikali mpya ya umoja wa taifa nchini Sudan ni hatua muhimu ya kuimarisha uhusiano wake na Marekani. Lakini ingawaje ni hivyo, lazima hatua zichukuliwe za kumaliza mgogoro wa Darfur ili vikwazo vilivyowekwa viweze kuondolewa. Bw. Zoellick amesema kuwa mapatano ya amani ya kusini mwa Sudan yaliyosainiwa mwezi wa Januari mwaka huu yanahitaji kupanuliwa hadi katika mgogoro mwingine wa Darfur. Bw. Zoellick amesema kuwa kuondolewa kwa vikwazo vya kiuchumi vilivyowekwa na Marekani mwaka 1997 kwa hoja kuwa serikali ya Sudan inaunga mkono vitendo vya kigaidi kumezungumziwa wakati wa mazungumzo yake na Viongozi wenzake wa Sudan. Naibu Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Marekani amemaliza kwa kusema kuwa nchi yake haiko tayari kuondoa vikwazo hivyo ingawaje vita vya wenyewe kwa wenyewe sasa vimemalizika kusini mwa Sudan.