1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UchumiMarekani

Marekani kutumbukia katika mzozo wa kiuchumi?

26 Septemba 2023

Miezi minne baada ya kunusurika na kushindwa kulipa madeni yake, Marekani, taifa linalotajwa kuwa na uchumi mkubwa zaidi ulimwenguni, liko tena kwenye ukingo wa kutumbukia katika mzozo mkubwa wa kifedha.

Wabunge wa Bunge la Marekani katika vikao vyake
Wabunge wa Bunge la Marekani katika vikao vyakePicha: Jonathan Ernst/REUTERS

Mara hii, sababu ni upinzani wa baadhi ya wabunge kwa msaada wa ziada wa mabilioni ya dola yanayotolewa na Washington kwa Ukraine inayopambana na uvamizi wa Urusi. 

Wabunge wa Democrat wana malumbano makali na wenzao wa Republican katika baraza la Congress juu matumizi ya ziada, ambayo kama hayakuidhinishwa kuwa sheria, basi yanaweza kusababisha kushindwa kwa serikali kufanya shughuli zake. 

Wabunge wa Marekani wamebakia na siku nne tu kutoka sasa wawe wameshafikia makubaliano, kabla ya ufadhili wa huduma za serikali haujamalizika.

Soma pia:Mbunge wa chama cha Democratic Menendez akutwa na maelfu ya dola nyumbani kwake na kukataa kwamba ni za rushwa

Ikiwa serikali itashindwa kulipia gharama za huduma zake, maelfu kwa maelfu ya wafanyakazi wake kwenye mbuga, makumbusho na maeneo mengine yanayoendeshwa kwa fedha za serikali kuu wataathirika. 

Na hilo halitamalizikia hapo, bali linaweza kuwa na athari mbaya za kisiasa kwa Rais Joe Biden anayetaka kuwania tena urais mwaka 2024.

Republican wakataa pendekezo la Biden

Wawakilishi wa chama cha Republican walikataa kuunga mkono viwango vya matumizi ya serikali vilivyokubaliwa kati ya Biden na Spika Kevin McCarthy, ambavyo vingeliweza kuifanya serikali iendelee kufanya kazi, ilisema Ikulu ya White House.

Spika wa Bunge la Marekani Kevin McCarthy akiwa na Rais Joe BidenPicha: Jacquelyn Martin-Pool/Getty Images

Siku ya Jumamosi, Biden alisemakundi dogo la Warepublican wenye misimamo mikali halitaki kuyaheshimu makubaliano hayo, kwa hivyo kila Mmarekani sasa atalazimika kuumia.

"Umefika wakati kwa Warepublican kuanza kufanya kazi waliyochaguliwa na Wamarekani kuifanya." Alisema Biden.

Wasiwasi wa sasa miongoni mwa wabunge wa Republican unatokana na msaada wa ziada kwa Ukraine, baada ya Volodymyr Zelensky kulitembelea baraza la Congress siku ya Alkhamis kuomba silaha zaidi kukabiliana na uvamizi wa miezi 18 wa Urusi.

Vyama vyote viwili kwenye baraza la Senetivinaunga mkono rasimu ya msaada wa dola bilioni 24, lakini baadhi ya wajumbe wa Republican kwenye Baraza la Wawakilishi wanatishia kuipinga rasimu hiyo.

Soma pia:Marekani imeahidi kutoa dola milioni 100 kwa Haiti

Mbunge Marjorie Taylor Greene, ambaye ni mshirika mkubwa wa rais wa zamani wa Marekani, Donald Trump, ametuma video kwenye ukurasa wa X, akisema ghataidhinisha  hata senti moja kwenda kwenye vita nchini Ukraine.

"Mimi ni Mmarekani Kwanza, naifanyia kazi Marekani. Nawafanyia kazi watu wa Marekani." Alisema

Kauli hiyo iliungwa mkono na mbunge mwenzake, Eli Crane, aliyesema kwamba Wamarekani wamechoka na kuwalipia fedha wengine, akipinga kile alichodai ni kutumia fedha kwa mambo ambayo hawana maslahi wala uwezo nayo.

Kundi hilo la wabunge linamuweka Spika McCarthy kwenye nafasi ngumu ya maamuzi. 

Kupitisha bajeti katika baraza la Congress

Kawaida, kura ya kupitisha bajeti hugeuka kuwa vita kwenye baraza la Congress, huku kila chama kikitumia uwezekano wa serikali kushindwa kulipia gharama zake kupata jambo kutoka mwengine.

Huwa wanaendelea na vita hivyo hadi dakika za mwisho mwisho ndipo wanapata suluhu la pamoja. 

Lakini mwaka huu, kiwango cha uhasama kimekuwa cha juu kuliko kawaida.

Kwenye baraza la Seneti, majibizano yanaongozwa na vigogo wawili, kiongozi wa wengi kutoka Democrat, Chuck Schumer, na kiongozi wa wachache, Mitch McConnell, wa Republican.

Endapo makubaliano hayakufikiwa, wabunge wanaweza kugeukia hatua za muda mfupi za ufadhili wa serikali, ambazo zitatowa ahueni ya kitambo huku wabunge hao wakisaka suluhisho la pamoja.

Soma pia:Marekani na Urusi zatoa mwito wa utulivu jimboni Nagorno Karabakh

Wasiwasi huu wa serikali ya Marekani kushindwa kupata pesa za kujiendesha unakuja ikiwa ni miezi minne tu baada ya mzozo wa ukomo wa kukopa.

Nchi hiyo iliponea chupuchupu kushindwa kulipa madeni yake, jambo ambalo lingepelekea janga kubwa kwa uchumi wa Marekani na wa dunia.