1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani kuwekea ushuru bidhaa za Umoja wa Ulaya

3 Oktoba 2019

Marekani itaziwekea ushuru wa asilimia 25 bidhaa zenye thamani ya dola bilioni 7.5 za Umoja wa Ulaya kuanzia Oktoba 18, kufuatia uamuzi wa shirika la biashara ulimwenguni, WTO.

Airbus bei Luftfahrtmesse in Paris-Le Bourget
Picha: picture-alliance/dpa/S. Suki

Kufuatia uamuzi wa WTO hapo jana kwenye shauri lililodumu kwa miaka 15 lililozingatia ruzuku za serikali kwa Airbus, afisa mwandamizi wa ofisi ya biashara nchini Marekani, amesema Marekani itaziwekea ushuru wa asilimia 10 ndege kutoka Umoja wa Ulaya, lakini hata hivyo hautahusu vifaa vya ndege.

Aidha, Marekani itaziwekea ushuru wa asilimia 25 bidhaa nyingine ambazo ni pamoja na za kilimo na viwanda. Afisa huyo wa biashara amewaambia waandishi wa habari kwamba ingawa uamuzi huo wa WTO unairuhusu Marekani kuiadhibu Umoja wa Ulaya kwa ushuru wa hadi asilimia 100, lakini Washington imeamua kutokwenda umbali huo, katika wakati inapotafuta suluhu wa mzozo huo wa muda mrefu.

Rais Donald Trump amesifu uamuzi huo wa WTO na kuita ni "ushindi mkubwa" kwa Marekani. Amesema Marekani imeshinda kwenye mashauri yake mengi ya WTO dhidi ya mataifa yaliyokuwa yanajinufaisha kwa muda mrefu kupitia mgongo wa Marekani. 

Rais Donald Trump amesifu hatua hiyo ya WTOPicha: Reuters/K. Lamarque

Wakati orodha ya mwisho ya bidhaa zitakazowekewa ushuru ikisubiriwa kutangazwa muda mfupi ujao, tayari Umoja wa Ulaya umetishia kwa kusema itajibu hatua yoyote itakayochukuliwa na Marekani.

Brussels imesema kupitia taarifa yake kwamba iwapo Marekani itaamua kuwekea ushuru bidhaa zake, itausukuma Umoja huo katika hali ambayo haitakuwa na chaguo jingine zaidi ya kujibu sawa kwa kuziwekea ushuru bidhaa za Marekani.

Hata hivyo ofisi ya biashara ya Marekani imesema hatua hiyo itakuwa ni kinyume chini ya kanuni za WTO na Marekani huenda ikajiandaa kujibu.

Shauri hilo lilianza mwaka 2004, wakati Washington ilipozituhumu Uingereza, Ufaransa, Ujerumani na Uhispania kwa kutoa ufadhili na ruzuku zisizo halali ili kusaidia uzalishaji wa bidhaa anuwai za Airbus. Tangu wakati huo kumekuwa na rufaa kadhaa ili kufikia suluhu ya mzozo huo uliokuwa mgumu kwa shirika la WTO.

Shauri hilo lilifunguliwa na tangu mwaka 2004 na kufuatiwa na rufaa kadhaaPicha: picture-alliance/Joker/M. Fejer

Ulaya yatishia kujibu hatua yoyote ya Marekani.

Lakini uamuzi wa jana ambao hauwezi kukatiwa rufaa ni wa kwanza unaoiruhusu Marekani chini ya sheria ya kimataifa ya biashara kuchukua hatua dhidi ya bidhaa ya Umoja wa Ulaya.

Huku tarehe ya mwisho ya Uingereza kujiondoa Umoja wa Ulaya ikiwa imekaribia Uingereza imesema kwenye taarifa yake kwamba haihusiki na vikwazo vyovyote vya Marekani vinavyowekwa dhidi ya Umoja huo na ilikuwa inatafuta uthibitisho kutoka WTO kwamba iliheshimu kikamilifu na maamuzi yote yaliyohusiana na Airbus.

Hata hivyo, afisa huyo wa biashara wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari kwamba Umoja wa Ulaya kwa ujumla wake inakabiliwa na kuwajibika na kushindwa kusuluhisha suala hilo la ruzuku, na kusisitiza kwamba hakuna atakayeepuka matokeo yake, huku pia akizitaja nchi zitakazokumbwa na kadhia hiyo ambazo zinaweza kuishawishi Brussels kuondoa ruzuku hizo kwa Airbus.

Katika hatua nyingine, Brussels nayo hivi karibuni itakuwa na fursa ya kuweka ushuru wake baada ya kuthibitishwa na shirika la WTO. Kwenye shauri tofauti lililofunguliwa mwaka 2005, Umoja wa Ulaya ulidai kampuni ya ndege ya Boeing ilipokea ruzuku iliyozuiwa ya thamani ya dola bilioni 19.1, kuanzia mwaka 1989 hadi 2006 kutoka ofisi mbalimbali za serikali ya Marekani.

Kufuatia madai hayo Brussels iliwaomba wasuluhishi wa WTO kuiruhusu kuziwekea ushuru bidhaa za Marekani za thamani ya dola bilioni 12.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW