Marekani: Matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula
9 Novemba 2022Dalili za awali zimeonyesha kuwa chama cha Republican kinaelekea kuchukua udhibiti wa Baraza la Wawakilishi, huku matokeo ya Baraza la Seneti yakikaribia pia kutangazwa kwani kura zilikuwa hazijahesabiwa katika baadhi ya majimbo.
Chama cha Democratic kimeshinda viti vya ugavana katika majimbo ya Michigan, Pennsylvania na Wisconsin jana Jumanne, na hivyo kuwawezesha kujilinda dhidi ya sheria ya majimbo yanayotawaliwa na Warepublican kuhusu masuala kama vile haki za uavyaji mimba na uchaguzi wa haki.
Majimbo hayo matatu yalipewa jina la "ukuta wa bluu" ambao ulimsaidia
Rais Biden kumpiku Donald Trump mnamo mwaka 2020, wakati maafisa wa Republican walipojaribu kutengua matokeo hayo kwa kura ya turufu.
Soma zaidi: Wamarekani wanapiga kura
Kwa ujumla, nafasi 36 za ugavana zilikuwa zikiwaniwa huko nchini Marekani katika uchaguzi huu wa katikati ya muhula, na mustakabali wa haki ya uavyaji mimba na usimamizi wa uchaguzi vikiwa hatarini katika uchaguzi huu wenye ushindani mkubwa.
Utafiti wa kituo cha Edison ulikadiria kuwa Wademocrats walikuwa mbele kwa viti viwili huku hatma ya viti vya Pwani ya Magharibi ikiwa bado haijaamuliwa. Chama cha Republican kimeonekana kupata ushindi katika maeneo muhimu ya Florida, Georgia na Texas.
WaRepublicans wana matumaini ya kushinda
Akizungumza na wafuasi wa chama usiku wa kuamkia leo, Kevin McCarthy, Kiongozi wa Republican katika Baraza la Wawakilishi alionekana mwenye matumaini makubwa ya kupata ushindi:
"Sasa ngoja niwaambie, mmetoka usiku mkubwa. Lakini mkiamka kesho, tutakuwa wengi bungeni na Nancy Pelosi atakuwa miongoni mwa wachache. Warepublican watafanya kazi na yeyote ambaye yuko tayari kuungana nasi kutoa mwelekeo huu mpya ambao umetakiwa na Wamarekani. Lakini hakuna wakati wa kupoteza. Kazi yetu inaanza sasa. Tuirejeshe Marekani kwenye njia sahihi. Asante, Mungu akubariki na usiku mwema."
Soma zaidi:Biden, Trump wafanya kampeni za mwisho kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula
Ingawa Wademocrats waliweza kuhifadhi viti katika Baraza la Wawakilishi katika maeneo ya Virginia hadi Kansas na Rhode Island, matokeo ya sasa yanaonyesha Warepublican wakipata tu viti vinane vya bunge, itatosha kuwapa udhibiti wa Baraza la Wawakilishi ikiwa hesabu ya kura italingana na makadirio ya uchaguzi.
Kihistoria, chama cha rais aliyeko madarakani kwa kawaida huwa hakifanyi vizuri katika uchaguzi wa katikati ya muhula. Utafiti wa maoni ya wapiga kura unaonyesha viwango vya chini vya ridhaa ya Wamarekani kwa Rais Biden, ambaye ameshughulikia mfumuko wa bei na kupanda kwa bei ya mafuta.