1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Iran zakutana kwa mara ya pili kuhusu Irak

24 Julai 2007

Nchi mbili mahasimu wa jadi Marekani na Iran zimefanya duru ya pili ya mazungumzo ya ana kwa ana mjini Baghdad, mazungumzo hayo yalihusu hali ya usalama wa Irak inayozidi kudidimia.

Raia wa Irak apitisha ujumbe wake kwenye bango
Raia wa Irak apitisha ujumbe wake kwenye bangoPicha: AP

Mazungumzo hayo ambayo sio ya kawaida kufanywa na nchi hizi mbili yalifanyika leo katika ofisi ya waziri mkuu wa Irak Nuri al Maliki ambae aliyafungua rasmi kwa hotuba fupi.

Bwana Malik katika hotuba yake alisema kuwa Irak ina matarajio makubwa ya kuungwa mkono na nchi hizi mbili katika kuleta utulivu nchini humo

Zaidi bwana Malik amesema kuwa nchi yake inayo haki ya kuwahusisha washirika wake katika vita vyake dhidi ya ugaidi.

Marekani iliwakilishwa na balozi wake wa nchini Irak Ryan Crocker huku ujumbe wa Iran nao ukiongozwa na balozi wake Hassan Kazemi Qomi.

Mkutano huo umefanyika huku Washington ikikabiliwa na shinikizo la kuhakikisha utulivu nchini Irak kabla ya baraza la Congres halijapokea taarifa ya muhimu kuhusu Irak inayotarajiwa kuwasilishwa mwezi Septemba.

Wakati mkutano huo ulipokuwa ukiendelea mshambuliaji wa kujitoa muhanga alishambulia kwa bomu la kutegwa ndani ya gari na kuwauwa takriban watu 26 huku watu wengine 70 wakijeruhiwa katika shambulio hilo.

Shambulio hilo lilitokea karibu na soko katika mji wa Washia wa Hilla ulio kilomoita 100 kusini mwa mji mkuu wa Baghdad.

Mkutano kama huo waleo uliwahi kufanyika tarehe 28 mwezi Mei ambao pia ulituwama katika hali ya usalama ya Irak huku ukiwayaweka kando maswala mbalimbali yanayosababisha mikwaruzano baina ya Marekani na Jamuhuri ya Kiislamu ya Iran.

Mkutano huo wa mwezi Mei hata hivyo haukufanikiwa kupata suluhisho kwani nchi zote mbili zilitetea hoja zake kwa dhati, Marekani ikiilaumu Iran kwa kuendeleza machafuko nchini Irak na Tehran nayo ikiitaka Washington iondoke kutoka Irak.

Marekani ilivunja uhusiano wake wa kidiplomasia na Iran tangu mwaka 1980 wakati iran iliouvamia ubalozi wa Marekani mjini Tehran na kuwashikilia mateka wanadiplomasia wake kwa siku 444.

Nchi hizi hazina maelewano mazuri kwa sababu chungu nzima ukiwemo mpango wa nyuklia wa Iran ambao Marekani inaamini kuwa hatimae Tehran inalenga kutengeneza silaha za nyuklia madai ambayo yanapingwa vikali na Iran.

Hata hivyo mazungumzo hayo yamezusha hisia mbali mbali kutoka kwa wanasiasa wa nchini Irak.

Mwanasiasa Mahmud Othman, Mkurdi anasema kuwa hategemei chochote hata baada ya mkutano huo wa leo kufanyika kwani pande zote mbili zina malengo yake binafsi.

Baadhi ya wanasiasa wanahimiza mikutano ya aina hiyo wanasema Wairak wenyewe wameshindwa kutatua matatizo ya kiusalama nchini mwao.

Nao viongozi wa Kishia wa Irak ambao wana uhusiano wa karibu na utawala wa Kishia wa Iran wanasema kuwa mkutano huo wa leo ni hatua yenye manufaa.