Marekani na Iran zaonekana kukaribia makubaliano
29 Mei 2026
Wawakilishi wa Marekani na Iran katika mazungumzo ya amani jana Alhamisi walifikia makubaliano ya muda ya kuongeza muda wa usitishaji vita ambavyo vimedumu kwa miezi 3 kwa siku 60 na kuanza duru mpya ya mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran. Haya ni kwa mujibu wa chanzo cha Marekani chenye ufahamu wa suala hilo.
Iran haikuthibitisha mara moja kuhusu makubaliano yoyote.
Makubaliano ya amani yanaonekana kuyumba
Rasimu hiyo inakuja wakati makubaliano dhaifu ya kusitisha mapigano kati ya nchi hiyo mbili yanaonekana kuyumba.
Mvutano wa hivi karibuni zaidi ulitokea chini ya siku moja iliyopita wakati Kuwait ilipodungua makombora yaliyorushwa kutoka Iran. Hii ni kulingana na Kamandi Kuu ya Marekani.
Yaliomo kwenye rasimu ya makubaliano
Chini ya makubaliano hayo yaliyoripotiwa, Iran ambayo imekuwa ikijaribu kudhibiti usafiri wa baharini kupitia Mlango-Bahari wa Hormuz na kutoza meli kwa ajili ya kupita, itafungua tena lango hilo kuelekea Ghuba.
Iran pia inatakiwa kuondoa mabomu yote ya baharini ambayo imeweka kwenye njia hiyo ya maji ndani ya siku 30 na kwa kubadilishana, jeshi la Wanamaji la Marekani litasitisha majaribio ya kuweka kizuizi cha safari za meli kwenda na kutoka bandari za Iran.
Pakistan kufahamishwa kuhusu makubaliano yatakapofikiwa
Lakini shirika la habari la Iran la Tasnim, likinukuu chanzo cha karibu na waakilishi hao wa Iran kwenye mazungumzo ya amani, kimesema rasimu hiyo haijakamilishwa na kwamba mpatanishi Pakistan atafahamishwa iwapo makubaliano yatafikiwa.
Vyanzo vya Iran vilivyonukuliwa na vyombo vya habari vya ndani vimesema makubaliano yoyote yatakamilika tu yatakapotangazwa na Tehran, huku Vance akisema uamuzi wa mwisho wa kuidhinisha au kutoidhinisha ni kutoka kwa Trump.
Iran inataka mali yake iliyofungiwa nje ya nchi kuachiwa
Tasnim pia imeripoti kuwa Iran inataka kuachiliwa kwa karibu dola bilioni 24 za mali ya Iran zilizofungiwa nje ya nchi kama sehemu ya makubaliano hayo.
Hakuna takwimu rasmi ya mali hiyo iliyofungiwa, ingawa hivi karibuni, vyombo vya habari vya Iran vilikadiria kiwango cha kati ya dola bilioni 100 na bilioni 123.
Kuhusu suala la mpango wa nyuklia, maafisa wa Iran wamesema litaahirishwa hadi wakati mwingine baada ya makubaliano juu ya rasimu hiyo.
Marekani yatakiwa kutoa hakikisho la kuzingatia makubaliano
Moja ya matakwa makuu ya Tehran ni hakikisho kwamba Washington itaheshimu makubaliano yoyote baada ya Marekani kujiondoa katika makubaliano ya nyuklia ya 2015 wakati wa muhula wa kwanza wa Trump madarakani.
Ikiwa pande zote zitafikia makubaliano, rasimu ya mwisho itawasilishwa kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kuidhinishwa, kiwango cha juu cha dhamana inayotambuliwa katika sheria za kimataifa.