Marekani na Israel zaishambulia Iran ambayo pia imejibu
28 Februari 2026
Vyombo vya habari vya Iran vimeripoti mashambulizi kote nchini humo. Miripuko kadhaa ya mabomu imesikika katika mji mkuu wa Iran huku shambulio la kwanza likiwa limefanyika karibu na ofisi za Kiongozi Mkuu wa Iran Ayatollah Ali Khamenei.
Haikubainika mara moja ikiwa Khamenei mwenye umri wa miaka 86 alikuwa ofisini mwake wakati wa mashambulizi hayo kwa kuwa hajaonekana hadharani kwa siku kadhaa tangu kuongezeka kwa mvutano kati ya nchi yake na Marekani ambayo imepelekea meli na ndege za kivita huko Mashariki ya Kati.
Trump na Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu wamesema kuwa baada ya mashambulizi hayo, Wairan wanapaswa kuchukua hatma yao mikononi mwao. Hata hivyo serikali ya Tehran imesema rais Masoud Pezeshkian yuko hai na salama. Iran pia imejibu kwa kushambulia kambi za jesh la Marekani katika mataifa ya Qatar, Bahrain na Umoja wa Falme za kiarabu.
Mashambulizi haya yanafanyika wakati mazungumzo yalikuwa yakiendelea ili kujaribu kuishinikiza Iran kufikia makubaliano kuhusu mpango wake wa nyuklia. Nchi jirani ya Iraq imetangaza kuifunga anga yake huku ving'ora vikisikika kote Israel baada ya jeshi la ulinzi IDF kutangaza kuwa mfululizo wa makombora yamefyetuliwa kuelekea Israel. Mashirika mbalimbali ya ndege yamesitisha safari zao huko Mashariki ya Kati.