1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Israel zajadili kupunguza kasi ya vita Gaza

15 Desemba 2023

Marekani inakubaliana na Israel kuwa mapambano dhidi ya Hamas yatachukua miezi kadhaa, lakini zinajadili ratiba ya Israel ya kujiondoa kwenye mapigano kwa kuwalenga viongozi wa kundi la wanamgambo wa Hamas.

Israel | Treffen Jake Sullivan mit Benjamin Netenjahu
Picha: GPO/Anadolu/picture alliance

Ijumaa 15.12.2023 ni siku ya 70 ya vita ambapo Israel imeendeleza mashambulizi yake huko Gaza dhidi ya wapiganaji wa kundi la Hamas hata baada ya Mshauri wa Usalama wa Taifa wa Marekani Jake Sullivan kukutana na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu na Waziri wake wa Ulinzi Yoav Gallant.  Sullivan amesema Marekani inaitaka Israel kuelekeza vita vyake katika Ukanda wa Gaza kwa kuwalenga viongozi wa Hamas tu katika operesheni yake ya kijeshi.

Kushoto: Mshauri wa Usalama wa Marekani Jake Sullivan alipokutana na Waziri wa Ulinzi wa Israel Yoav Gallant mjini Tel Aviv Desemba 14.2023.Picha: GPO/Anadolu/picture alliance

Mshauri huyo wa Usalama wa Taifa wa Marekani, Jake Sullivan amewaambia waandishi wa habari wakati wa ziara yake nchini Israel kwamba kutakuwepo na kipindi cha mpito kwenda kwenye awamu nyingine ya vita hivi, ambayo itawalenga moja kwa moja na kwa usahihi viongozi wa Hamas kwa kuhusisha zaidi taarifa za kijasusi.

Soma:Israel yakabiliwa na ukosoaji kufuatia vita huko Gaza

Sullivan amesema amejadili juu ya wakati huo wa mpito katika mikutano na Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu, baraza la mawaziri wanaosimamia vita na wakuu wa kijeshi. Walengwa wakuu wa vita vya Israeli ni pamoja na Mohammed Deif, kiongozi wa kijeshi wa Hamas ambaye ndio mpangaji mkuu wa mashambulizi ya Oktoba 7 dhidi ya Israel, mkuu wake wa pili, Marwan Issa na kiongozi mwingine wa Hamas aliyeko Gaza, Yahya Sinwar.

Kufuatia mazungumzo na maafisa wa Israel, mshauri wa maswala ya usalama wa taifa wa Marekani, Jake Sullivan amekutana na Rais wa mamlaka ya Palestina, Mahmoud Abbas kujadili mustakabali wa eneo lililozingirwa baada ya vita, ambalo, kulingana na afisa mkuu wa Marekani, inawezekana kujumuisha kuvirejesha vikosi vya usalama vya Palestina vilivyo fukuzwa na Hamas kutoka Gaza mnamo mwaka 2007 ilipoudhibiti Ukanda wa Gaza.

Rais wa mamlaka ya Palestina Mahmoud Abbas picha ilipigwa wakati wa mkutano wa dharura wa Jumuiya ya Nchi za Kiarabu na Jumuiya ya Ushirikiano wa Kiislamu (OIC), mjini Riyadh, Saudi Arabia Jumamosi, Novemba 11, 2023,Picha: Saudi Press Agency/Newscom/picture alliance

Wakati huo huo makumi ya wanawake wa Israel walikusanyika katika uwanja wa Habima mjini Tel Aviv leo Ijumaa kutoa wito wa kusitishwa mara moja kwa vita kati ya Israel na Hamas. Wanawake hao waliovalia mavazi meupe, wakiwa wamebeba mabango yenye maneno ya Kiingereza, Kiarabu na Kihebrania, walikaa kimya wakiashiria kupinga kile wanachosema ni utamaduni unaozuia mazungumzo ya amani na maridhiano.

Soma:Waziri wa ulinzi wa Israel nchi hiyo inahitaji miezi kadhaa kushinda vita katika ukanda wa Gaza

Wakati huo huo, Mahakama ya Uholanzi leo imetupilia mbali matakwa ya mashirika ya kutetea haki za binadamu ya kuizuia serikali ya Uholanzi kuiuzia Israel vipuri vya ndege za kivita za aina ya F-35 ambayo mashirika hayo yalisema vinawezesha uhalifu wa kivita katika Ukanda wa Gaza uliozingirwa.

Majaji katika Mahakama ya The Hague wamesema ni lazima kuiachia serikali ya Uholanzi uhuru wake wa masuala ya kisiasa na kisera katika kuamua mauzo ya nje ya silaha.

Vyanzo: DPA/RTRE/AP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW