1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Japan zatoa tahadhari ya kutokea tsunami

Daniel Gakuba
15 Januari 2022

Japan na Marekani zimewataka watu wanaoishi kwenye mwambao wa bahari ya Pasifiki kuelekea sehemu za miinuko, kutokana na kitisho cha tsunami baada mripuko wa volkano ya chini ya bahari karibu na kisiwa cha Tonga.

Tonga - Vulkan Ausbruch
Picha za Satelaiti kuonyeesha mripuko wa volkano ya chini ya bahari karibu na kisiwa cha TongaPicha: Japan Meteorolog/AP/picture alliance

Picha za satelaiti zimeonyesha mripuko wa volkano hiyo ya Hunga Tonga-Hunga Ha'apai, ambao umerusha angani moshi na majivu katika umbo la uyoga mkubwa, na kusababisha tetemeko katika eneo la bahari ya Pasifiki linalokizunguka kisiwa cha Tonga.

Soma zaidi: Japan yaadhimisha miaka 10 ya janga la tsunami

Taarifa za taasisi ya hali ya hewa ya Australia zinasema mawimbi yenye kima cha mita 1.2 yalishuhudiwa katika mji mkuu wa Tonga wa Nuku'alofa.

Japan pia imeripoti kuwa mawimbi yaliyotokana na tsunami hiyo yamefika kwenye pwani yake, yakiwa na kima cha hadi mita tatu.

 Watu wahaha wakitafuta sehemu za miinuko    

Hali hiyo imesababisha taharuki na watu wa kisiwa kidogo cha Tonga walionekana wakikimbia mbio kuhamia kwenye maeneo ya vilima.

Alama ya buluu kwenye ramani inaonyesha ilipo volkano iliyoripuka na kusababisha tsunami

Mmoja wao, Mere Taufa amesema wakati volkano iliporipuka alikuwa nyumbani akijiandaa kwa mlo wa mchana, na aligutushwa na mawimbi ya bahari yaliyoanza kuivamia nyumba yake.

''Lilikuwa tetemeko kubwa sana lililoitikisa ardhi. Kaka yangu alidhani ni mabomu yaliyokuwa yakiripuliwa karibu na nyumba yetu,'' alisema Taufa akizungumza na tovuti ya Stuff News.

Soma zaidi: Tsunami yaua 40, yaharibu majengo 600 Indonesia

Mkazi huyo amesema nyumba yao ilifurika maji katika muda wa dakika chache, na kuongeza kuwa aliuona ukuta wa nyumba ya jirani yake ukiporomoka.

''Bila kukawia tulijua kuwa ni tsunami imetokea, kwa kiwango cha maji yaliyoivamia nyumba yetu. Ungeweza kuwasikia watu wakipiga mayowe kila mahali, wakikimbilia maeneo salama, kila mmoja akitafuta sehemu iliyoinuka.''

Muungurumo mithili ya mabomu na radi

Mripuko huo wa volkano ya chini ya bahari ulidumu kwa takribani dakika nane, na umekuja muda mfupi baada ya kutolewa kwa tahadhari ya tsunami nyingine.

Picha hii ya maktaba inaonyesha pwani ya Samoa baada ya tsunami ya Septemba 2009Picha: AP

Kulingana na duru kutoka mji wa Suva, mripuko huo ulisikika kama miungurumo ya radi katika kisiwa cha Fiji kilicho umbali wa kilomita 800 kutoka kitovu chake, na mawimbi makubwa yaliipiga pwani ya kisiwa hicho.

Miito ya tahadhari imetolewa pia New Zealand, American Samoa, Vanuatu, Chile na Australia.

Onyo la tsunami lilitolewa pia kwa watu waishio pwani ya magharibi ya Marekani, kuanzia California hadi Alaska.

Soma zaidi: Idadi ya watu waliokufa Indonesia yaongezeka hadi 1,407

Katika tangazo lake, kitengo cha Marekani cha tahadhari dhidi ya Tsunami kimewaonya watu wanaoishi katika maeneo yanayokabiliwa na kitisho, kikisema ''tsunami inakuja, na kumbukeni kuwa mawimbi ya mwanzo hayaonekani makubwa sana. Ondoka kwenye mwambao muhamie kwenye miinuko.''

Canada pia imetoa angalizo kama hilo kwa watu wa mkoa wa British Columbia, ikiwaasa kuepuka kwenda ufukweni.

 

Vyanzo: afpe, ape

      

  

     

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW