Marekani na Korea Kusini kufanya luteka kubwa ya kijeshi
3 Machi 2023Katika mkutano wa pamoja na waandishi habari, maafisa wa jeshi kutoka Korea Kusini na Marekani wamesema Ijumaa kuwa luteka hiyo ya siku 10 itakayofanyika kuanzia Machi 13 hadi 23 na iliyopewa jina ''Ngao ya Uhuru'', inalenga kuimarisha uwezo wao wa ulinzi na nguvu ya pamoja ya kujihami.
Kanali Lee Sung Jun, msemaji wa Kamandi ya majeshi ya Korea Kusini amesema majeshi ya Korea Kusini na Marekani yataandaa mafunzo hayo, wakati wakijiandaa na uchokozi wowote unaoweza kufanywa na jeshi la Korea Kaskazini.
Mazoezi kuzingatia uchokozi wa Korea Kaskazini
''Luteka hii itaangazia zaidi uchokozi wa Korea Kaskazini kama vile kitisho cha kutumia nyuklia na mpango wake wa makombora, pamoja na mafunzo tuliyoyapata kutokana na vita na mizozo ya hivi karibuni, na kubadilika kwa mazingira ya kiusalama,'' alifafanua Kanali Lee.
Mazoezi yaliyopita ya kijeshi yaliibua hisia kali kutoka kwa Korea Kaskazini, ambayo imekuwa ikurusha makombora pamoja na kutoa kitisho cha kutumia nyuklia. Korea Kaskazini imesema luteka kama hiyo ya pamoja ni ushahidi kwamba Marekani na washirika wake wanasababisha uchokozi.
Kuna uwezekano kwamba Korea Kaskazini ikajibu mazoezi yajayo ya Korea Kusini na Marekani kwa kufanya majaribio ya kombora kwa sababu inayachukulia mazoezi hayo kama maandalizi ya vita vya uchokozi.
Kwa upande wake Kanali Isaac L. Taylor, msemaji wa jeshi la Marekani amesema wakati wa luteka hiyo, washirika hao pia wataendesha mafunzo ya jeshi la ardhini, yanayoitwa Ngao ya Shujaa FTX, ili kuimarisha uwezo wao wa kutekeleza operesheni.
''Pia tutafanya mazoezi kadhaa ya pamoja ya nchi kavu, ambayo yamerudi katika kiwango kikubwa cha mazoezi ya kivita yaliyopewa jina la 'Foal Eagle'. Mojawapo ya mazoezi ni pamoja na luteka ya meli ambayo itafanywa kuimarisha uwezo wa utekelezaji wa operesheni,'' alibainisha Kanali Taylor.
Korea Kaskazini nayo itafanya luteka ya msimu wa baridi
Korea Kusini na Marekani zimekuwa zikitanua luteka yao ya kijeshi katika kukabiliana na vitisho vya nyuklia vya Korea Kaskazini. Maafisa wa Korea Kusini wamesema pia Korea Kaskazini inafanya luteka ya kijeshi ya kila mwaka ya wakati wa majira ya baridi.
Mwaka uliopita, Korea Kaskazini ilirusha zaidi ya makombora 70, ambayo ni makombora mengi zaidi kuwahi kutokea kwa mwaka mmoja, na mengine kadhaa yamefyatuliwa mwaka huu. Makombora mengi yalifanyiwa majaribio ya silaha zenye uwezo wa nyuklia, ambayo yametengenezwa kuweza kuishambulia Marekani na Korea Kusini.
Jeshi la Marekani limeionya Korea Kaskazini kwamba matumizi ya silaha za nyuklia yatasababisha mwisho wa utawala wa nchi hiyo. Aidha, Korea Kaskazini imesema njia pekee ya kupunguza mvutano katika Rasi ya Korea ni kwa Marekani kuachana na mipango yake ya kupeleka vifaa vya kimkakati Korea Kusini na kusitisha luteka za pamoja na mshirika wake huyo wa Asia.
(AP, Reuters)