Marekani na Korea Kusini zafanya luteka ya pamoja
15 Juni 2023Marekani na Korea Kusini zimefanya luteka ya pamoja ya kijeshi iliyoikasirisha Korea Kaskazini ambayo imejibu kwa kufyetua makombora mawili ya masafa marefu.
Rais Yoon Suk Yeol wa Korea Kusini alishuhudia luteka hiyo iliyofanyika kwenye mji wa kaskazini mashariki wa Pocheon kama sehemu ya maadhimisho ya miaka 70 ya kuundwa kwa jeshi la nchi hiyo.
Jumla ya wanajeshi 2,500 wameshiriki mazoezi hayo yaliyojumuisha urushaji wa ndege mamboleo za kivita chapa F35 na F16 pamoja na mifumo ya kisasa ya kufyetua makombora.
Sehemu ya mazoezi hayo ilikuwa ni kuonesha njia za kukabiliana na vitisho vya makombora ya nyuklia ya Korea Kaskazini na shambulizi kutoka nchi hiyo.
Korea Kaskazini imeitaja luteka hiyo kuwa "uchokozi" na imerusha makombora mawili kuonesha upinzani wake.