Marekani na Marafiki wa Syria wanautambua muungano wa upande wa upinzani wa Syria
12 Desemba 2012Tangazo hilo limetolewa kabla ya mkutano wa mjini Marakesh nchini Moroko kati ya viongozi wa makundi ya upinzani na nchi 130 zinazojiita "marafiki wa Syria" wanaowaunga mkono waasi tangu walipoanza mapambano yao March mwaka jana.
"Ni hatua muhimu" amesema Rais Barack Obama wakati wa mahojiano pamoja na kituo cha televisheni cha ABC.
Kwa namna hiyo Marekani inajiunga na Ufaransa, Uingereza, Uturuki na mataifa ya Ghuba yaliyokuwa ya mwanzo kuutambua muungano wa taifa la Syria mwezi uliopita.
"Tumeamua muungano wa upinzani wa Syria umejiandaa vya kutosha kuwawakilisha wananchi wa Syria kwa namna ambayo tunawaangalia kama wawakilishi halali wa umma wa Syria dhidi ya utawala wa Assad," amesema Rais Obama.
Urusi, mshirika wa jadi wa serikali ya Syria imeukosoa uamuzi huo na kuituhumu Washington kutaka kukorofisha kuwepo kipindi cha mpito nchini Syria. "Marekani inalenga moja kwa moja ushindi wa kijeshi wa muungano wa upinzani dhidi ya vikosi vya Bashar al Assad", amesema Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Urusi, Serguei Lavrov.
Katika wakati ambapo tangazo la rais wa Marekani linapewa umuhimu mkubwa katika juhudi za kuwahalalisha waasi machoni mwa jumuia ya kimataifa, mkutano wa Marrakesh hauonyeshi kama utafikia uamuzi wowote wa kutolewa msaada wa kijeshi au fedha wa moja kwa moja kwaajili ya waasi, ingawa nao pia umeutambua muungano huo wa upinzani.
Wawakilishi wa mataifa 130 wanaokutana Marrakesh nchini Moroko maarufu kwa jina la "Marafiki wa Syria" wametangaza pia hivi punde kuutambua muungano wa taifa kuwa mwakailishi pekee halali wa umma wa Syria. "Kwa sasa hakuna la ziada," amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Ufaransa, Laurent Fabius, anayehudhuria mkutano wa Marakesh, aliyeondowa uwezekano wa kupatiwa silaha waasi angalao kwa sasa.
Nchini Syria kwenyewe mapigano yanajongelea katikati ya mji mkuu Damascus yanakokutikana makaazi ya Rais Assad. Rami Abdulrahman wa shirika linalochunguza masuala ya haki za binaadam nchini Syria anasema kwamba sasa nchi hiyo inaharibiwa kabisa:"Nionavyo mie, na haya ni maoni yangu mie, tukiendelea kama hivi, hatutouvuruga utawala wa Assad. Tutaivuruga Syria."
Watu wasiopungua 40 elfu wameuwawa tangu vuguvugu la mageuzi lilipoanza Machi mwaka jana nchini Syria.
Mwandishi: Hamidou Oummilkheir/Reuters/AFP
Mhariri: Mohammed Khelef