1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroMamlaka ya Palestina

Marekani na Qatar kufanikisha mpango wa makubaliano Gaza?

15 Novemba 2023

Wakati mataifa mbalimbali duniani yakiendelea kutoa wito wa usitishwaji mapigano, wapatanishi kutoka Qatar wamesema Jumatano kuwa wanalenga kufanya mazungumzo na pande zote ili hatimaye kufikia makubaliano hayo.

US-Außenminister Antony Blinken besucht Jordanien
Waziri wa mambo ya nje wa Marekani Antony Blinken (kushoto) akisalimiana na Waziri Mkuu na waziri wa masuala ya kigeni wa Qatar Sheikh Mohammed bin Abdulrahman bin Jassim Al-Thani wakati wa mazungumzo ya kutafutia suluhu mzozo wa Gaza yaliyofanyika huko Amman, Jordan: (04.11.2023). Marekani na Qatar wameratibu pia mpango huu wa makubaliano kati ya Israel na Hamas.Picha: Jonathan Ernst/AP/picture alliance

Mpango huo utawezesha uwasilishwaji zaidi wa misaada ya kibinaadamu, usitishwaji mapigano kwa muda wa siku tatu na kuachiliwa huru kwa mateka wa Israel wapatao 50 kutoka huko Gaza.

Mpango huo wa makubaliano ambao bado unajadiliwa na ulioratibiwa na Marekani, utapelekea pia serikali ya Tel-Aviv kuwaachilia idadi isiyojulikana hadi sasa ya wanawake na watoto wa Kipalestina kutoka jela za Israel, lakini pia kuongeza kiasi cha msaada wa kibinadamu kinachoruhusiwa kuingia Gaza.

Ikiwa mpango huo utafikiwa, itakuwa ni mara ya kwanza kwa Hamas tangu shambulio lao la Oktoba 7, kuwaachilia idadi kubwa ya mateka inaowashikilia.

Mpango huo utaitaka pia Hamas kutoa orodha kamili ya mateka ambao bado wako hai huko Gaza lakini mpango huo hautojadili suala la kuachiwa mateka wote.

Wanajeshi wa Israel wakiendesha doria nje ya hospitali ya al-shifa huko Gaza (15.11.2023), harakati za kijeshi za Israel ndani ya hospitali hiyo zimeibua wasiwasi na ukosoaji mkubwa kimataifa.Picha: Israeli Defence Forces/REUTERS

Kulingana na Afisa aliye karibu na mazungumzo hayo, Kundi la Hamas tayari limeafiki mpango huo, tofauti na Israel ambayo bado inaendeleza majadiliano kuhusu vipengee kadhaa. Hata hivyo serikali ya Qatar, Israel na hata uongozi wa Hamas wote wamekataa kuzungumzia hadharani mpango huo.

Lakini Israel imesema hii leo kuwa: "Hata kama tutahitajika kusitisha mapigano ili kuwarudisha mateka wetu, hakutakuwa na usitishwaji kamili wa mapigano na vita hadi tufikie malengo yetu."

Soma pia: Miili iliyoanza kuharibika yazikwa katika kaburi la pamoja Gaza

Wakati hayo yakiripotiwa, Jeshi la Israel limeendeleza mashambulizi sehemu mbalimbali huko Gaza na limefahamisha kuwa limebomoa nyumba za wanamgambo huko Jerusalem mashariki. Wapalestina huko Jabalia wamekuwa wakijaribu kuiondoa miili chini ya vifusi baada ya shambulio la Israel.

" Hakika imetosha! Mpwa wangu alienda kutafuta maji kwa ajili ya familia yake, na sasa tumemkuta maiti chini ya kifusi. Inatosha! Mola tuhurumie! Tunahitaji suluhisho. Maiti zimetapakaa mitaani. Inaonekana maisha ya wanyama yana thamani zaidi kuliko maisha yetu," amesema mmoja wa wakazi huko Jabalia.

Miito ya usitishwaji mapigano na ukosoaji kwa Israel

 

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu na masuala ya dharura, Martin Griffiths ametoa wito wa kuchukuliwa hatua za haraka za "kusitisha mauaji"  huko Gaza.

Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la misaada ya kiutu na masuala ya dharura, Martin Griffiths Picha: Martial Trezzini/dpa/Keystone/picture alliance

Mawaziri wa Ulinzi wa Jumuiya ya Mataifa ya Kusini Mashariki mwa Asia (ASEAN) wakiwa katika mkutano huko Jakarta, wametoa wito wa usitishwaji mapigano huko Gaza na kuutaka Ulimwengu kushirikiana ili kuanzisha njia salama za usafirishaji misaada ya kibinadamu huko Gaza.

Naye Waziri Mkuu wa Uhispania Pedro Sanchez, ameitaka Israel kukomesha "mauaji ya kiholela ya Wapalestina" huko Gaza, ikiwa ni ukosoaji wake mkali zaidi kwa Tel Aviv tangu kuanza kwa vita hivyo.

Lakini Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan ambaye anatarajiwa katika siku mbili zijazo kufanya ziara nchini Ujerumani na kukutana na  Kansela Olaf Scholz, amekuwa na tamko kali na kusema Israel ni "taifa la kigaidi" linaloendesha uhalifu wa kivita na kukiuka sheria za kimataifa huko Gaza, kauli iliyoibua ukosoaji mkubwa kutoka Israel na washirika wake wa Magharibi.