Marekani na Saudia zaishambulia Irak
29 Julai 2026
Saudi Arabia imethibitisha kuhusika katika mashambulizi hayo yaliyowalenga wanamgambo walio na mafungamano na Iran. Saudia imesema mashambulizi hayo ni jawabu la mashambulizi ya droni yaliyolenga miundo mbinu ya mafuta huko Sharqiya na Riyadh. Wizara ya Ulinzi ya Saudi Arabia katika ujumbe iliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa X imesema imefanya hivyo kutokana na "haki yake ya kujilinda."
Haya yanafanyika baada ya Marekani kusema imetibua "shambulizi la kushtukiza" la Iran lililofanyika baada ya siku chache za utulivu baina ya nchi hizo mbili. Kulingana na Kamandi Kuu ya Marekani CENTCOM, imezuia mashambulizi ya makombora ya Iran Jumanne, ikidai makombora hayo yalikuwa yanavilenga vikosi vya Marekani huko Mashariki ya Kati.
CENTCOM ambayo haikusema hasa makombora hayo yalipolengwa, inasema licha ya kuyazuia mashambulizi yote, vikosi vya Marekani vinasalia macho na tayari kwa makabiliano.
Mashambulizi haya ya sasa yanafikisha mwisho usitishwaji mapigano wa muda uliodumu kwa siku kadhaa.
Mazungumzo "mazuri" kuwahi kufanyika na rais wa Marekani
Wakati huo huo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na Rais Donald Trump huku maafisa kutoka pande zote mbili za viongozi hao wakisifu ushirikiano wa serikali hizo mbili baada ya mkutano wa faragha uliodumu kwa dakika 90.
Kikao hicho ambacho ndicho cha kwanza baina ya viongozi hao wawili tangu kuanza kwa vita vya Marekani na Israel dhidi ya Iran, hakikujulikana matokeo yake kabla Netanyahu hajahudhuria misa ya wafu ya seneta Lindsey Graham.
Lakini baada ya kikao hicho, ikulu ya White House imeyaelezea mazungumzó baina ya viongozi hao wawili kama "mazuri na ya kujenga."
Katika video iliyochapishwa kwenye mtandao wa kijamii baada ya mkutano huo, Netanyahu amekiita kikao hicho kama "mojawapo ya mazungumzo mazuri zaidi ambayo amewahi kuyafanya na rais wa Marekani" akiongeza kuwa yamegusia lengo lao moja ambalo ni kuhakikisha kuwa Iran haipati silaha za nyuklia.
Mkutano huu unakuja huku uchaguzi Israel ukinukia na shirika la habari la Reuters limesema kuwa Netanyahu alikuwa analenga kupata uungwaji mkono wa Trump katika kampeni yake ya kuchaguliwa tena Oktoba 27.
Leseni ya kuunda mifumo ya ulinzi ya Patriot
Hayo yakiarifiwa Rais Donald Trump amefanya kikao pia na Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy ambapo wamejadili kuhusu kuanzisha upya mazungumzo ya amani na Urusi na mipango ya Ukraine kuunda mifumo ya Patriot ya kuzuia makombora.
Kikao cha Trump na Zelenskiy pia kilikuwa cha faragha kabla rais huyo wa Ukraine hajakutana na Rais wa Finland Alexander Stubb katika hoteli moja ya Washington na baada ya hapo akaelekea kukutana na maseneta wa Marekani.
Zelenskiy ambaye amekuwa akiwashinikiza marafiki wa Ukraine kuipa nchi yake msaada wa mifumo ya kuzuia makombora ya angani, amesema katika ujumbe aliouandika kwenye mtandao wa kijamii wa Telegram kuwa, alikuwa na mkutano "mzuri" na Trump na kwamba wamejadiliana kuhusiana na ahadi ya Trump kwa Ukraine katika mkutano wa kilele wa NATO mapema mwezi huu, kuipa Ukraine leseni ya kuunda mifumo yake ya Patriot ya kuzuia makombora.
Vyanzo: AP/AFP/Reuters