1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroYemen

Marekani na Uingereza zashambulia ngome za wahouthi, Yemen

12 Januari 2024

Marekani, Uingereza na nchi nyingine 8 washirika wamefanya mashambulizi ya pamoja ya anga dhidi ya maeneo kadhaa yanayodhibitiwa na waasi wa Houthi nchini Yemen.

Mzozo wa Yemen | Mashambulizi ya anga dhidi ya waasi wa Houthi
Ndege za kivita zilizotumiwa katika operesheni ya Marekani na Uingereza dhidi ya Waasi wa Houthi nchini Yemen: 12.01.2024Picha: US Central Command via X/REUTERS

Serikali za Australia, Bahrain, Canada, Denmark, Ujerumani, Uholanzi, New Zealand, Jamhuri ya Korea, Uingereza na Marekani zimeeleza katika taarifa ya pamoja hii leo kuwa lengo lao ni kupunguza hali ya mvutano na kurejesha utulivu katika Bahari ya Shamu, lakini wakasisitiza kuwa hawatosita kuyalinda maisha ya watu na kukabiliana na vitisho ili kuhakikisha usafirishaji wa biashara katika moja ya njia muhimu zaidi ya majini duniani. 

Mataifa hayo yamesema hatua hiyo ni katika dhamira ya kurejesha hali ya utulivu kwenye  Bahari ya Sham.  

Soma pia:Mashambulizi ya anga ya Marekani na Uingereza yalenga maeneo ya Wahouthi Yemen

Mashambulizi hayo ya angani ambayo yamehusisha ndege na meli za kivita, manowari na makombora yameilenga miji kadhaa ya Yemen inayodhibitiwa na waasi hao. Karibu maeneo 60 ya Wahouthi yamelengwa ikiwa ni pamoja na kamandi za kundi hilo, ghala za silaha, bohari, mifumo ya ulinzi wa anga na vifaa mbalimbali.

Ndege ya kivita ya Marekani ikielekea kwenye operesheni dhidi ya waasi wa Houthi huko YemenPicha: Royal Air Force/dpa/picture alliance

Waasi wa Houthi wamesema katika taarifa kuwa mashambulizi hayo ya uchokozi yamesababisha vifo vya wapiganaji wao watano huku wengine sita wakijeruhiwa. Msemaji wa tawi la kijeshi la waasi wa Houthi Yehya Saree ameapa kulipiza kisasi:

"Maadui zetu wa Marekani na Uingereza wanawajibika kikamilifu kwa uchokozi wao wa kijinai dhidi ya watu wetu wa Yemen, na uchokozi huo hautaachwa bila kujibiwa wala kuadhibiwa."

Soma pia: Baraza la Usalama lapitisha azimio la kulaani mashambulizi ya Wahouthi

Hatua ya mataifa hayo inafuatia mashambulizi ya hivi karibuni ya waasi wa Houthi wanaoungwa mkono na Iran ambayo wameyafanya dhidi ya meli za kibiashara katika Bahari ya Sham.

Msimamo wa Marekani, Uingereza na Urusi

Helikopta ya kijeshi ya waasi wa Houthi ikielea juu ya meli ya mizigo ya Galaxy Leader huku wapiganaji wa Houthi wakitua kwenye meli hiyo katika Bahari ya Sham: 20.11.2023. Picha: Houthi Military Media/REUTERS

Katika taarifa yake, Rais wa Marekani Joe Biden ameyataja mashambulizi hayo kuwa ni "jibu la moja kwa moja" kwa mashambulizi "yasiyokuwa ya kawaida" ya Wahouthi, na kwamba hawatosita kuchukua hatua zaidi endapo itahitajika.

Lakini Waziri wa Ulinzi wa Uingereza James Heappey amesema mashambulizi hayo yamefanyika katika hatua ya kujilinda na kwamba serikali mjini London inafahamu umuhimu wa kuzuia mzozo kusambaa katika eneo hilo na kusisitiza kuwa kwa sasa hawana mpango wa kuendeleza operesheni hiyo.

Soma pia: Azimio la UN la laani hujuma za waasi wa Houthi

Urusi ambayo ni mshirika mkuu wa Iran imelaani mashambulizi hayo ya Marekani na Uingereza dhidi ya waasi wa Houthi nchini Yemen na kusema yanalenga kusababisha uharibifu na kuchochea kutanuka kwa mzozo huko Mashariki ya Kati baada ya vita vya Israel dhidi ya kundi la Hamas katika Ukanda wa Gaza kulitikisa eneo hilo. Moscow imeitisha hii leo mkutano wa dharura wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa ili kujadili suala hilo.

Vyanzo: (Mashirika)