Marekani na Ujerumani kujadili misaada kwa Ukraine
5 Septemba 2024Maafisa wa ngazi za juu wa jeshi la Marekani wanatarajiwa kuhudhuria mkutano wa kimataifa utakaojadili msaada wa kijeshi kwa ajili ya Ukraine wakati ambapo Urusi imefanya shambulio baya kabisa la makombora na wakati ambapo majeshi ya Ukraine yanaendeleza shinikizo kwenye jimbo la Urusi la Kursk.
Waziri wa ulinzi wa Marekani Lloyd Austin, ataongoza mkutano huo wa nchi zaidi ya 50 zinazoiunga mkono Ukraine.
Mkuu wa majeshi wa Marekani pia atashiriki kwenye mkutano huo utakayofanyika kwenye kambi ya kikosi cha anga cha Ramstein, kusini magharibi mwa Ujerumani.
Ukraine mara kwa mara imekuwa inaomba msaada zaidi wa kijeshi na ruhusa ya kutumia silaha za masafa marefu.
Mkutano huo unafanyika baada ya Urusi kutumia makombora mawili ya masafa marefu kukilenga chuo cha kijeshi na kusababisha vifo vya watu zaidi ya 50.
Watu wengine zaidi ya 270 waliheruhiwa. Hospitali iliyopo karibu na chuo hicho pia ililengwa.