Marekani na Ulaya zapanga mikakati ya kupambana dhidi ya IS
23 Novemba 2015Kerry amesema hayo huku shughuli za kawaida zikiendelea kukwama Brussels, Ubelgiji kutokana na kitisho cha mashambulizi ya kigaidi kama yaliyotokea Paris.
Matamshi hayo ya waziri wa mambo ya nje wa Marekani yanakuja kabla ya mazungumzo yanayotarajiwa hapo kesho kati ya Rais wa Marekani Barack Obama na mwenzake wa Ufaransa Francois Hollande mjini Washington kuhusu mikakati ya kupambana dhidi ya wanamgambo wa IS.
IS limedai kufanya mashambulizi ya Paris yaliyotokea tarehe 13 mwezi huu ambapo kiasi ya watu 130 waliuawa na wengine 350 walijeruhiwa. Kerry amesema Rais Obama amemuomba kila mmoja katika serikali yake kuja na mawazo mapya ya namna ya kuliangamiza kundi la IS.
Ufaransa,Marekani na Uingereza kushirikiana zaidi
Waziri mkuu wa Uingereza David Cameron amesema anaamini kuwa nchi yake inapaswa kufanya mashambulizi ya angani wakishirikiana na Ufaransa na nchi nyingine washirika nchini Syria katika juhudi za kulitokomeza kundi la IS.
Waziri huyo mkuu wa Uingereza amesema baadaye wiki hii, atatafuta ridhaa ya bunge la nchi yake kuidhinisha mkakati huo wa vita dhidi ya IS. Kwa upande wake, Hollande waliyekutana leo na Cameron mjini Paris amesema Ufaransa inapanga kuongeza mashambulizi ya anga dhidi ya ngome za wanamgambo wa IS nchini Syria.
Kiongozi huyo wa Ufaransa wiki hii anatarajiwa kutafuta ushirikiano zaidi kutoka viongozi wengine katika mapambano dhidi ya IS baada ya mashambulizi ya Paris. Akitoka mjini Washinton, ataelekea Moscow kukutana na Rais wa Urusi Vladimir Putin.
Hayo yanakuja huku askari wa Ubelgiji wakiwamata watu wengine watano katika misako dhidi ya washukiwa wa ugaidi. Idadi ya waliokamatwa katika misako hiyo kufikia sasa imefikia 21.
Mkwamo Brussel kutokana na hofu ya ugaidi
Shughuli za kawaida katika mji mkuu wa Ubelgiji, Brussels zimekwama kwa siku ya tatu mfululizo tangu siku ya Jumamosi kutokana na kitisho cha kufanyika mashambulizi makubwa ya kigaidi kama yale yaliyotokea Paris.
Ofisi ya mwendesha mashitaka wa Ubelgiji imesema kufuatia operesheni zilizofanya jana usiku katika maeneo ya mji wa Brussels na eneo la Liege, watu watano walikamatwa na jumla ya watu 21 wanahojiwa na polisi huku hakimu akitarajiwa kutoa uamuzi baadaye leo iwapo watasalia kuzuiwa na polisi au wataachiwa huru.
Kiasi cha euro 26,000 zilipatikana katika misako hiyo miongoni mwa vitu vingine vinavyofanyiwa uchunguzi na polisi. Mmoja wa washukiwa wakuu wa mashambulizi ya Paris, raia wa Ubelgiji Salah Abdeslam mwenye umri wa miaka 26 mpaka sasa hajakamatwa licha ya misako hiyo chungu nzima. Inahofiwa kuwa mshukiwa huyo anajificha Ubelgiji na huenda amejihami.
Mwandishi: Caro Robi/Reuters/dpa/afp/ap
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman