Marekani na Urusi kuijadili Syria
14 Oktoba 2015Waziri wa Ulinzi wa Marekani Ash Carter ameyatangaza mazungumzo hayo kuwa ni ya "kumaliza tofauti" wakati huu ambao madege ya kivita ya pande zote mbili, Marekani na Urusi yanafanya mashambulizi katika maeneo ya vita ya taifa hilo la Mashariki ya Kati.
Akizungumza muda mfupi baada ya kufanya majadiliano na waziri mwenzake wa ulinzi wa Australia mjini Boston, Carter alisema Urusi lazima ifanye operesheni zake kitaalumu katika anga ya Syria na vilevile kujifungamanisha kanuni za msingi za kiusalama.
Mkutano kuendelea zaidi
Aidha waziri huyo aliendelea kusema watafanya mkutano mwingine wenye maudhui hayo hayo kesho. Mjadala wa suala hilo ni jambo la kuendelea kwa kuwa mpaka wakati huu hakuna maafikiano. Amesema pamoja na kuendelea kutokubaliana kisera kuhusu Syria, lakini watakuwa tayari angalau kukabiliana kuhusiana na usalama wa watu wao wa anga katika maeneo hayo ya operesheni.
Waziri Carter amesema yeye hana wajibu wa kupanga muda wa kuhitimisha mazungumzo hayo lakini ana matarajio ya kumalizika katika kipindi kifupi kijacho.
Hata hivyo ameonya kuwa mazungumzio ya kijeshi kati ya pande hizo mbili huenda yasifanikiwe kufadili msimamo wa Urusi kuelekea hatua zake za kijeshi nchini Syria , ambao ni wenye makosa na mtazamo potovu kimkakati .
Mashambulizi ya Urusi
Urusi hapo jana ilisema jeshi lake la angani katika kipindi cha masaa 24 liliyashambulia maeneo 86 ya kigaidi, yakiwemo kadhaa yenye wapiganaji wa kundi la wanamgambo wa Dola la Kiislamu. Marekani na washirika wake ambao wanajihusisha vita vya angani nchini humo wameituhumu Urusi kwa kuwalenga waasi wenye msimamo wa wastani wanaoungwa mkono na Marekani na kutaka kuuongezea nguvu utawala wa rais Bashar al-Assad.
Katika hatua nyingine msemaji wa kundi la Dola la Kiislamu amethibitisha kwa njia ya sauti iliyorekodiwa kwamba kiongozi namba mbili wa kundi hilo ameuwawa na mashambulizi ya angani ya Marekani yalitokea mapema mwaka huu.
Msemaji huyo, Abu Mohammed al-Adnani amesikika akisema "Wamarekani wanafuraha kwa kumuuwa Abu Mutaz al Qurashi na kufikiria ni ushindi kwao..tunawaeleza bado hajafa. Ameacha mashujaa watakaopambana na Marekani na washirika wake. Taarifa yake ilisambazwa na tovuti yenye mfungamano na kundi la Dola la Kiislamu ya al-Furqan.
Agosti 21, mwaka huu Marekani ilitangaza Qurashi, ambae vilevile alijulikana kama Fadhil Ahmad al-Hayali, aliwawa Agosti 18 kwa makombora yake ya angani karibu na mji wa kaskazini wa Iraq wa Mosul.
Mwandishi: Sudi Mnette DPA/ AFPE
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman