Marekani na Urusi zakubaliana kusitisha mapigano Syria
8 Julai 2017Rais wa Marekani Donald Trump na rais Vladimir Putin wa Urusi jana Ijumaa walikubaliana mpango wa kusitisha mapigano katika maeneo ya kusini na magharibi mwa Syria , ikiwa ni jaribio la hivi karibuni kabisa la kusitisha umwagikaji wa damu katika nchi hiyo iliyoharibiwa kwa vita.
Makubaliano hayo yataanza kutekelezwa mchana saa za Syria siku ya Jumapili, wanadiplomasia wa ngazi ya juu wa Urusi na Marekani wamesema wataka wakitangaza makubaliano hayo yaliyofikiwa na viongozi wao pembezoni mwa mkutano wa kilele wa kundi la mataifa yaliyoendelea na yanyoinukia kiuchumi G20 nchini Ujerumani.
"Ni mafanikio yetu ya kwanza ," amesema waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Rex Tillerson akizungumzia ushirikiano baina ya Ikulu ya Marekani White House na Kremlin.
Shirika linaloangalia haki za binadamu nchini Syria limesema makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yalikuwa yanatarajiwa kujumuisha miji ya Daraa, Sweida na Queitra.
Limesema katika taarifa iliyotolewa jana Ijumaa kwamba makubaliano hayo yatashuhudia kuondolewa kwa majeshi ya serikali ya Syria kutoka katika mstari wa mbele na kurejea katika makambi.
Wakimbizi kurejea nyumbani
Eneo hilo litatayarishwa kuwapokea wakimbizi wa Syria kutoka Jordan. Pia ina maana ya kuruhusu misaada wa kiutu kuwasili katika eneo hilo.
Vita nchini Syria , ambayo hivi sasa vimo katika mwaka wa saba , vimeyaingiza mataifa makubwa duniani ikiwa ni pamoja na Marekani na Urusi.
Wakati huo huo polisi walisumbuka kuweza kuwadhibiti waandamanaji waliokuwa wakifanya ghasia wakati maelfu ya waandamanaji wenye msimamo mkali wa mrengo wa kushoto walifanya fujo katika mji wa Hamburg , ambako Ujerumani ni mwenyeji wa mkutano wa G20.
Kansela Angela Merkel alishutumu ghasia hizo na kusema ,"hazikubaliki," akiongeza kwamba alikuwa "anatambua maandamano ya amani" lakini maandamano ya ghasia yanahatarisha maisha ya watu."
Mkutano wa G20 ulianza rasmi jana Ijumaa na uliandamana na maandamano ya ghasia yaliyofanywa na wanaharakati wa mrengo wa kushoto tangu ulipoanza.
Mapema jana waandamanaji walilazimisha rais wa Marekani Donald Trump kubadilisha njia kuelekea katika mkutano huo wa kilele, na mkewe Melania , hakuweza kushiriki katika mpango wa mkutano wa wake wa marais kwasababu polisi ilisema ilikuwa si salama kwake kuondoka katika nyumba alipofikizia.
Polisi pia walisema waandamanaji 20 walishambulia walinzi wa usalama katika hoteli ya Park Hyatt mjini Hamburg , ambayo amefikzia rais wa Urusi Vladimir Putin , Moon Jae In wa korea kusini na waziri mkuu wa Australia Malcom Turnbull.
Mwandishi : Sekione Kitojo / dpae
Mhariri: Josephat Charo