Marekani, Urusi zatakiwa kuhakikisha vita vinasitishwa Syria
28 Aprili 2016Di Mistura ameyasema hayo baada ya kuwa na kikao na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuliarifu kuhusu duru ya hivi karibuni ya mazungumzo ya kutafuta amani Syria.
Mjumbe huyo maalumu wa Umoja wa Mataifa amesema mazungumzo hayo yalipiga hatua licha ya kuongezeka kwa ghasia nchini Syria ambazo zinatishia kufikiwa makubaliano ya kuvimaliza vita vya Syria.
Di Mistura ameitaka Marekani ambayo inayaunga mkono makundi kadhaa ya waasi nchini Syria na Urusi ambayo ni mshirika mkubwa wa utawala wa Rais wa Syria Bashar al Assad kuitisha mkutano wa ngazi ya juu wa mawaziri wa nchi zenye nguvu zaidi duniani kujadili namna ya kuheshimiwa kwa makubaliano ya kusitisha mapigano kabla ya mazungumzo ya kutafuta amani kuendelea.
Mapigano yamezidi Syria
Tangazo hilo linakuja huku majeshi ya serikali ya Syria yakiishambulia hospitali na maeneo ya makaazi ya watu katika mji wa Aleppo na kusababisha vifo vya takriban watu 20 wakiwemo watoto wawili.
Daktari pekee wa kuwatibu watoto katika mji huo wa Aleppo ambao unadhibitiwa na waasi pia ameuawa katika mashambulizi hayo ya angani yaliyofanywa hapo jana.
Katika mashambulizi mengine mashariki na magharibi mwa mji huo mapema hapo jana watu 16 waliuawa wakiwemo raia watano.
Di Mistura amesema pande zote zilizoshiriki mazungumzo ya Geneva sasa zanatambua haja ya kuwepo serikali ya mpito Syria ambayo itakuwa na jukumu la kuandika katiba mpya hata kama kuna tofauti kubwa kuhusu muundo wa serikali hiyo.
Di Mistura ameongeza kuwa kuna uelewa mzuri kuwa kipindi cha mpito kinapaswa kusimamiwa na serikali mpya ya kuaminika na inayojumuisha kila upande ambayo itachukua mahala pa serikali ya sasa.
Hata hivyo mjumbe huyo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Syria amekataa kuzungumzia suali kuu ambalo limekuwa kikwazo cha mazungumzo kusonga mbele nalo ni hatma ya Rais Assad.
Je Assad ataachia madaraka?
Upande wa upinzani umesiistiza kuwa Assad hawezi kuwa sehemu ya serikali mpya ya mpito na sharti akubalie kuachia madaraka kama sehemu ya makubaliano. Upinzani unaoungwa mkono na Saudi Arabia na nchi za magharibi, ulijiondoa rasmi kutoka kwenye mazungumzo wiki hii ukipinga kuongezeka kwa ghasia.
Upande wa serikali nao umesema Assad hawezi kuwa mojawapo ya ajenda ya mazungumzo ya kutafuta amani.
Hapo jana Urusi iliutaka Umoja wa Mataifa kuliweka kundi la wapiganaji la Jaish al Islam katika orodha ya makundi ya kigaidi kwa madai lina mafungamano na kundi la wanamgambo wenye itikadi kali la Dola la Kiislamu IS na mtandao wa kigaidi wa Al Qaeda.
Mazungumzo ya kutafuta amani yamekuwa yakilenga kuvimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe ambavyo vimesababisha vifo vya zaidi ya watu 270,000 na kuwaaacha mamilioni ya Wasyria bila ya makaazi.
Mwandishi: Caro Robi/afp
Mhariri: Gakuba Daniel