1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani na Urusi zatunishiana misuli Venezuela

2 Mei 2019

Mzozo wa kuwania madaraka nchini Venezuela kati ya Rais Nicolas Maduro na spika wa bunge, Juan Guaido, unazidi kufukuta, huku Urusi na  Marekani zikichukuwa nafasi yao kwenye taifa hilo la Amerika ya Kusini.

Sergei Lawrow und Mike Pompeo
Picha: picture-alliance/dpa/AP/A. Zemlianichenko

Siku ya Jumatano (Mei 1) Guaido aliitisha tena maandamano ya umma kwenye mitaa ya mji mkuu Caracas, lakini waandishi wa habari walioko huko walisema vyombo vya usalama hadi sasa vimefanikiwa kudhibiti hali na wengi wa wanajeshi hawakuitikia wito wake wa kuungana na wenzao walioasi kumpindua Maduro. 

Guaido alisema kungelifanyika kile alichokiita "maandamano makubwa kabisa" kwenye historia ya Venezuela na kwamba tayari mamilioni ya raia walikuwako mitaani kwenye awamu ya mwisho ya kumuondoa Maduro, lakini wengi wa waandamanaji waliondoka mitaani na kurejea majumbani mwao.

Rais Maduro aliwahutubia wafuasi wake, akikanusha vikali kauli ya Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, kwamba rais huyo alikuwa tayari kuachia madaraka na kukimbilia nchini Cuba, lau si uingiliaji kati wa Urusi.

Maduro alisema viongozi wa Marekani ulikuwa unadanganywa na wapinzani wake ili kuwasaidia njama ya kumuondoa, lakini hilo lisingelifanikiwa.

Rais Nicolas Maduro akiwahutubia wafuasi wake mjini Caracas.Picha: Reuters/F. Torrealba

"Jaribio lile la mapinduzi ambalo lilifanyika jana, upuuzi huo wa kupindua uliongozwa moja kwa moja kutoka Ikulu ya Marekani, na John Bolton. Hicho ndicho ninachokilaani na kutaka hatua hizi haramu na jaribio la mapinduzi la John Bolton dhidi ya demokrasia ya Venezuela lichunguzwe ndani ya Marekani." Aliwaambia wafuasi hao.

Marekani na Urusi kwenye mzozo

Kikosi maalum cha ulinzi wa rais kiliwatawanya waandamanaji waliokuwa wamekataa kuondoka mitaani hapo jana, kikitumia gesi ya kutoa machozi, ambapo waandishi wa habari wa Reuters wanasema mtu mmoja alijeruhiwa.

Makundi ya haki za binaadamu yalisema mwanamke mmoja alifariki dunia wakati akifanyia upasuaji kufuatia kupigwa risasi kichwani mjini Caracas. 

Mkwamo huu wa kisiasa nchini Venezuela unaongeza mzozo kati ya Marekani na Urusi, zinazotuhumiana kuingilia mambo ya ndani ya taifa hilo mwanachama wa Umoja wa Nchi Zinazozalisha Mafuta kwa wingi duniani, OPEC.

Utawala wa Rais Trump wa Marekani umeiwekea vikwazo serikali ya Maduro na imekataa kuondosha uwezekano wa kuivamia Venezuela kijeshi, licha ya kusema inapendelea zaidi kuwepo kwa kipindi cha mpito kwa njia ya amani. 

Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mike Pompeo, hapo jana alikiambia kituo cha Fox Business Network kuwa matumizi ya jeshi yanawezakana. 

Mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov, alisema kuwa hatua yoyote zaidi ya uchokozi nchini Venezuela itakabiliwa na matokeo mabaya kabisa.

Reuters, AFP

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW