Marekani na Uturuki zajadili hali ya Kaskazini mwa Syria
15 Januari 2019Marekani na Uturuki leo zimejadili juu ya hatima ya wapiganaji wa kikurdi nchini Syria ambao ni washirika wa Marekani. Marekani imesisitiza kwamba wapiganaji hao hawapaswi kushambuliwa, wakati Uturuki imepinga kinachoonekana kuwa vitisho vya Marekani vya kuiadhibu Uturuki kiuchumi ikiwa itathubutu kuwashambulia wapiganaji hao.
Rais wa Uturuki Recep Erdogan amepania kuwashambulia wapiganaji hao wa Kikurdi wa kundi la YPG. Hali hiyo ya kutokukubaliana iliyojitokeza baina ya Marekani na Uturuki, ni matokeo ya uamuzi wa rais Trump aliotangaza tarehe 19 mwezi uliopita juu ya kuyaondoa majeshi yake kutoka Syria ikiwa na maana ya kuwaacha wapiganaji hao wa Kikurdi katika hatari wakati ambapo Uturuki inatafakari kufanya mashambulio kaskazini mwa Syria.
Waziri wa mambo ya nje wa Uturuki Mevlut Cavusoglu amesema hatua ya Marekani kuiwekea nchi yake vitisho vya kiuchumi haitasaidia chochote. Uhusiano kati ya Uturuki na Marekani umekwaruzika kutokana msaada wa Marekani kwa wapiganaji wa Kikurdi ambao Uturuki inawazingatia kuwa kundi la magaidi linalofungamana na chama cha Wakurdi cha PKK ambacho kimepigwa marufuku nchini Uturuki.
Kwa muda wa miongo kadhaa chama hicho kimekuwa kinapigania kuwa na jimbo lake huru ndani ya Uturuki. Wapiganaji wa Kikurdi wa YPG wamekuwa washirika wa Marekani katika harakati za kupambana na magaidi wanaojiita dola la Kiislamu IS nchini Syria na wanadhibiti maeneo makubwa kaskazini mwa Syria.
Rais Erdogan anadhamiria kuwashambulia wapiganaji hao baada ya rais Trump kutangaza kwamba atayaondoa majeshi yake kutoka Syria.Trump alifahamisha mwishoni mwa wiki iliyopita kwamba zoezi linaanza la kuwaondoa wanajeshi hao ambao walipelekwa Syria ili kusaidia katika harakati za kuwatimua magaidi wanaojiita dola la kiislamu IS. Hata hivyo Trump amesema Marekani itaendelea kuwatandika magaidi hao endapo italazimu kufanya hivyo.
Uturuki imevipinga vitisho hivyo vinashoashiria kuzorota upya kwa uhusiano baina ya nchi mbili hizo wanachama wa jumuiya ya kijeshi ya NATO. Msemaji wa rais nchini Uturuki ameeleza kuwa magaidi hawawezi kuwa washirika wa Marekani. Ameeleza kuwa anatumai Marekani itaheshimu ushirikiano wa kiulinzi iliyonao na Uturuki.
Mwandishi:Zainab Aziz/RTRE
Mhariri: Yusuf Saumu