Marekani: Rwanda na DRC zatoa rasimu ya mpango wa amani
6 Mei 2025
Dhamira ya juhudi hizo za Washington ni kumaliza machafuko kwenye eneo lenye utajiri mkubwa wa madini la mashariki mwa Kongo.
Taarifa za kupokelewa kwa rasimu hizo imetolewa na mshauri mwandamizi wa Rais Donald Trump kuhusu masuala ya Afrika na Mashariki ya Kati, Massad Boulos.
Afisa huyo hakuweka wazi kile kilichopendekezwa na pande hizo mbili lakini amesema kuwasilishwa kwa rasimu hizo ni "hatua muhimu" kwenye mchakato unaoendelea.
Hayo yamejiri baada ya mwezi uliopita waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani, Marco Rubio kushuhudia Rwanda na Kongo zikitia saini makubaliano ya kufanya kazi pamoja kufikia mkataba wa amani.
Soma pia: Tshisekedi akutana na mshauri wa Trump mjini Kinshasa
Hata hivyo hakukuwepo maelezo zaidi juu ya rasimu hiyo na ikiwa ingeliruhusu Marekani kujipatia madini muhimu ya Kongo, jambo ambalo Rais Felix Tshisekedi amelitaja mara kadhaa ili kupata usaidizi wa Marekani katika kuumaliza mzozo huo uliodumu kwa miongo kadhaa na kusababisha maafa makubwa.
Pande hizo mbili zimekuwa zinalaumiana kwa machafuko mashariki mwa Kongo, huku serikali mjini Kinshasa ikiilaumu mara zote Rwanda kuwaunga mkono waasi wa M23 wanaopigana na vikosi vya serikali. Rwanda imekuwa ikikanusha madai hayo.