Marekani: Syria yaandaa shambulio la silaha za sumu
27 Juni 2017Ikulu ya Marekani imesema maandalizi ya shambulio hilo yanafanana na yale yaliofanywa na utawala wa Assad kabla ya kile kilichonekana kuwa lilikuwa shambulio la silaha za sumu katika mji uliokuwa ukishikiliwa na waasi hapo mwezi wa Aprili.
Serikalli ya Marekani ilichukuwa hatua ya kulipiza kisasi kwa kufanya shambulio la kombora kutoka kwenye meli yake ya kivita dhidi ya kambi ya kikosi cha anga cha Syria ambapo imesema shambulio hilo la silaha la sumu ndiko lilikotokea.
Shambulio hilo kwa kutumia makombora chapa 59 ya Tomehawk lilikuwa shambulio la kwanza kabisa la moja kwa moja la Marekani kwa utawala wa Syria na hatua kali kabisa ya Trump tokea aingie madarakani hapo mwezi wa Januari.
Hatua hiyo pia imepelekea kudhoofika kwa uhusiano kati ya Marekani na Urusi ambayo imeishutumu Marekani kwa kuvunja sheria ya kimataifa.
Urusi imekuwa ikiuunga mkono utawala wa Assad tokea mwaka 2015 kwa kufanya mashambulizi ya anga dhidi ya kile ilichosema wapiganji wa Kiislamu wa itikadi kali.
Onyo kali
Msemaji wa serikali ya Marekani Sean Spicer amesema katika taarifa hapo Jumatatu usiku kwamba "Marekani imegunduwa maandalizi ya uwezekano wa kufanyika kwa shambulio jengine la silaha za sumu na utawala wa Assad ambalo litasababisha mauaji makubwa kwa raia wakiwemo watoto wasiokuwa na hatia"
Taarifa hiyo ya kurasa mbili haikutowa ushahidi wowote ule kuhalalisha onyo hilo kali.Taarifa imesema harakati zinazofanyika ni sawa na maandalizi yaliofanywa na utawala huo kabla ya shambulio lake la silaha za sumu hapo April 4 mwaka 2017.
Shambulio hilo lilotuhumiwa kuwa la silaha za sumu katika mji uliokuwa ukishikiliwa na waasi wa KhanYunis limeuwa takriban watu 87 wakiwemo watoto wengi na taswira za watu waliokufa na wahanga waliokuwa wakiteseka na athari za shambulio hilo kumepelekea shutuma za kimataifa.Wizara ya mambo ya nje ya Marekani ilisema shambulio hilo lilikuwa ni uhalifu wa vita.
Maafisa wa wizara hiyo ya mambo ya nje ya Marekani ambapo kwa kawaida huwa wangelihusika na kutowa tangazo kubwa kama onyo hilo dhidi ya serikali ya Syria wamesema wameshtukizwa.
Uingereza yaunga mkono hatua ya kijeshi
Waziri wa ulinzi wa Uingereza Michael Fallon ameliambia shirika la utangazaji la Uingereza BBC Jumanne asubuhi kwamba ataunga mkono hatua ya kijeshi ya Marekani pindipo Syria itafanya shambulio hilo la silaha za sumu.
Ameongeza kusema kwamba kama inavyokuwa daima katika vita hatua za kijeshi zinazotumika lazima zihalalishwe,zizingatie sheria,ziwe za kiwango kinachostaki na kuwa na ulazima wa kufanya hivyo kama ilivyokuwa lilipofanyika shambulio la mwisho la sumu.
Mjini Moscow Franz Klintsevich naibu mwenyekiti wa tume ya ulinzi katika baraza la juu la bunge la Urusi amesema onyo hilo la Marekani linaashiria shambulio jipya dhidi ya vikosi vya Syria kwa kisingizio cha maandalizi ya nchi hiyo kujiandaa kufanya shambulio la silaha za sumu.
Mwandishi : Mohamed Dahman/AFP
Mhariri:Mohammed Abdul-Rahman