1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Ufichuzi wa Bolton waipa nguvu kesi dhidi ya Trump

Daniel Gakuba
28 Januari 2020

Kufuatia kuvuja kwa kitabu cha John Bolton akisema Trump alimtaka kusitisha msaada kwa Ukraine, hadi itakapomchunguza Joe Biden, imewafanya baadhi ya maseneta wa Republican kuunga mkono hoja ya kumualika kutoa ushahidi.

USA Präsident Donald Trump und Sicherheitsberater John Bolton
Picha: Getty Images/AFP/B. Smialowski

Wajumbe wa chama cha Democratic katika kesi inayoendelea dhidi ya Rais wa Marekani kwenye baraza la seneti, wamezidisha shinikizo la kutaka aliyekuwa mshauri mkuu wa Rais Donald Trump kuhusu usalama wa taifa, John Bolton, aitishwe kutoa ushahidi.

Hayo ni baada ya kuvuja kwa sehemu ya kitabu alichokiandika Bolton, ambamo anasema alitakiwa na Trump kusitisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, hadi itakapokuwa imeanzisha uchunguzi dhidi ya Makamu wa zamani wa rais nchini Marekani, Joe Biden.

Ufichuzi huo wa John Bolton katika kitabu chake ambacho bado hakijazinduliwa rasmi, umebadilisha mahesabu ya mawakili wa Trump ambao walitaka kesi dhidi ya mteja wao ihitimishwe haraka iwezekanavyo.

Pigo kwa hoja za upande wa utetezi

Madai ya mshauri huyo wa zamani wa masuala ya usalama, yanapinga hoja ya upande wa utetezi, ambao hadi wakati huu unashikilia kuwa hakuna shahidi yeyote ambaye amejitokeza, akieleza kuwa na ujuzi wa moja kwa moja, kwamba Trump alitaka kuufungamanisha msaada wa kijeshi kwa Ukraine, na nchi hiyo kuwachunguza wapinzani wake.

Ken Starr, mmoja wa watetezi wa Rais Donald TrumpPicha: AFP/US Senate TV/HO

Katika kesi inayomkabili, Rais Donald Trump anatuhumiwa kutumia vibaya madaraka yake, kwa kumshinikiza rais wa Ukraine kumchunguza makamu wa rais wa zamani Joe Biden, wakati Washington ikiushikilia msaada muhimu kwa nchi hiyo. Biden anaweza kuwa mpinzani wake mkuu wa Trump katika uchaguzi wa rais baadaye mwaka huu. Trump anashitakiwa pia kulizuia bunge kutekeleza majukumu yake.

Baadhi ya Warepublican washawishiwa

Madai ya Bolton ambaye alifukuzwa kazi na Trump baada ya kutofautiana kimtazamo, yamewafanya baadhi ya maseneta wa chama cha Republican kubadilisha mawazo, na kutafakari kuunga mkono rai ya Wademocrat kutaka kuwasikiliza mashahidi, rai ambayo hadi sasa Warepublican wamekuwa wakiipinga vikali. Mmoja wa Warepublican hao ni Seneta Mitt Romney, ambaye anasema hayuko peke yake.

Mitt Romney, seneta Mrepublican anayesema kuna haja ya kusikiliza ushahidi wa BoltonPicha: picture-alliance/dpa/T. Smart

''Nadhani Warepublican wengine wanaweza kujiunga na sisi ambao tunaamini tungepaswa kumsikiliza John Bolton'', amesema Romney na kuongeza, ''kama wapo mashahidi wengine na nyaraka nyingine, hilo ni suala tofauti, lakini umuhimu wa ushahidi wa Bolton katika kutusaidia kufanya maamuzi unazidi kuwa wa dhahiri.''

Upande wa utetezi wa Trump unatarajiwa kuhitimisha hoja zake leo Jumanne. Hapo jana, wanasheria maarufu Ken Starr na Alan Dershowitz walishambulia ushahidi uliowasilishwa na Wademocrat, wakisema mchakato mzima wa kumfungulia mashtaka Rais Trump hauna msingi wowote.

Wakati kesi dhidi yake ikiendelea, Rais Donald Trump anatarajia baadaye leo kutangaza mpango wake uliosubiriwa kwa muda mrefu, kuhusu suluhisho la mzozo kati ya Israel na Palestina. Mpango huo lakini tayari umekwishakataliwa na Wapalestina hata kabla haujazinduliwa rasmi.

 

ape, afpe

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW