1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Marekani, Uingereza na EU zalaani mauaji kwa watoa misaada

2 Aprili 2024

Mataifa yenye nguvu duniani yamelaani shambulizi la anga la majeshi ya Israel katika Ukanda wa Gaza ambapo wafanayakazi saba wa shirika la misaada la World Central Kitchen (WCK) waliuawa.

Gari lililoshambuliwa la Shirika la Misaada la World Central Kitchen (WCK)
Gari lililokuwa na wafanyakazi waliouawa wa Shirika la Misaada la World Central Kitchen (WCK)Picha: Ali Jadallah/Anadolu/picture alliance

Marekani, Uingereza na Umoja wa Ulaya zimeongoza katika ukosoaji wa kimataifa hii leo Jumanne kuhusu mashambulizi ya anga yaliyofanywa na jeshi la Israel katika Ukanda wa Gaza ambapo wafanyakazi saba wa shirika la misaada la World Central Kitchen waliuawa walipokuwa wakipakua misaada hiyo iliyohitajika sana katika eneo la Gaza lenye vita.

Mkuu wa maswala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep Borrell leo amelaani mauaji hayo na amesema kinachotokea leo hii huko Gaza ni kwamba ubinadamu umeshindikana. Utu umepoteza uhalisia wake. Kwa sababu si tetemeko la ardhi, sio mafuriko bali watu wanakufa kwa milipuko ya mabomu.

Mkuu wa maswala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya Josep BorrellPicha: John Thys/AFP/Getty Images

Borrell ameserma njia pekee ya kukomesha janga hili la kibinadamu ni kwa Israel kuwaheshimu zaidi raia na pia iruhusu msaada zaidi kuingia Gaza. Katika salamu zake za rambirambi kutokana na kuuawa wafanyakazi wa shirika la misaada la WCK katika Ukanda wa Gaza ametoa mwito wa kufanywa uchunguzi.

Amesisitiza umuhimu wa kuwalinda binadamu wote pamoja na wafanyakazi wa mashirika ya misaada. Mkuu huyo wa maswala ya kigeni wa Umoja wa Ulaya amesema mmoja kati ya wafanyakazi wa WCK waliouawa ni raia kutoka Poland ambayo ni mwanachama wa Jumuiya ya Umoja wa Ulaya.

Misri na Jordan zalaani mashambulio ya anga ya Israel

Wakati huo huo Misri pia imelaani mauaji ya wafanyakazi hao saba wa shirika la kutoa misaada katika Ukanda wa Gaza. Wizara ya Mambo ya Nje  katika taarifa yake imetoa wito wa kufanyika uchunguzi na pia kuiwajibisha Israel kwa kukiuka sheria za kimataifa na sheria ya kimataifa ya haki za binadamu. Mfalme Abdullah wa Jordan amelaani mashambulizi hayo ya anga yaliyowalenga wafanyakazi wa WCK. 

Kwa upande wake Uingereza imesema inataka maelezo kamili na ya uwazi kuhusu mashambulio hayo mabaya dhidi ya wafanyakazi wa shirika la misaada katika Ukanda wa Gaza. Waziri wa Mambo ya Nje wa Uingereza David Cameron, amesema raia mmoja wa Uingereza ni miongoni mwa wafanyakazi hao saba waliouawa. 

Waziri Mkuu wa Ireland anayeondoka Leo Varadkar, amesema kabla ya Mkutano wa Umoja wa Ulaya unaofanyika huko mjini Brussels, kwamba Israeli imo katika hatari ya kupoteza uungwaji mkono wa kimataifa kutokana na mashambulizi ya kigaidi ya Hamas mnamo Oktoba 7.

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin NetanyahuPicha: Maya Alleruzzo/AP/dpa/picture alliance

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema mashambulio hayo hayakukusudiwa. Msemaji wa jeshi la Israel (IDF) kamanda Daniel Hagari amesema kwenye ujumbe wa video kwamba Jeshi la Israel litafanya uchunguzi kuhusu shambulizi la anga lililosababisha kuuawa wafanyakazi saba wa shirika la misaada katika Ukanda wa Gaza na ameahidi kuonesha matokeo kwa uwazi.

Kamanda Hagari ametoa rambirambi za jeshi la Israel kwa mpishi mashuhuri Jose Andres, mwanzilishi wa shirika la misaada la World Central Kitchen (WCK) lenye makao yake makuu nchini Marekani ambalo wafanyakazi wake saba wameuawa.

Msemaji huyo wa jeshi la Israel ameeleza kwamba shirika la WCK lilikuwa mojawapo kati ya mashirika ya kwanza ya misaada yaliyowasaidia Waisraeli baada ya mauaji ya Oktoba 7, yaliyofanywa na kundi la Hamas.

Umoja wa Mataifa watahadharisha baa la njaa Gaza

Wakati hayo yakiendelea mashirika ya Umoja wa Mataifa yanaendelea kutahadharisha kwamba eneo la kaskazini mwa Gaza linakaribia kukumbwa na baa la njaa, na kuitaja hali hiyo kuwa ni mgogoro unaosababishwa na binadamu.

Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulika na Idadi ya Watu (UNFPA) katika Ukanda wa Gaza Dominic Allen, ameelezea hofu yake juu ya kinachoweza kutokea iwapo vita vitaendelea. Ameliambia shirika la habari la AFP kuwa hali inazidi kuwa mbaya huku watu walio na njaa wakiendelea kukabiliwa na uhaba wa chakula na dawa.

Vyanzo: DPA/AFP

 

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW