1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Uingereza zamuunga mkono Mark Rutte kuiongoza NATO

22 Februari 2024

Marekani na Uingereza zimetanagaza Alhamisi kumuunga mkono Waziri Mkuu wa Uholanzi anayeondoka Mark Rutte kumrithi Jens Stoltenberg kama katibu mkuu ajaye wa NATO, na kumweka katika nafasi kubwa ya kunyakua wadhifa huo.

Waziri Mkuu wa muda wa Uholanzi Mark Rutte
Waziri Mkuu wa Uholanzi Mark Rutte alitangaza mwaka jana kuachana na siasa za nchi hiyo.Picha: Omar Havana/AP/dpa

Mrithi wa Stoltenberg atakapoondoka madarakani mwezi Oktoba atachukua wadhifa huo katika kipindi muhimu, akiwa na jukumu la kuendeleza uungaji mkono wa wanachama wa NATO kwa utetezi ghali wa Ukraine dhidi ya uvamizi wa Urusi huku akilinda dhidi ya kuongezeka kwa mzozo huo ambako kunaweza kuutumbukiza muungano huo moja kwa moja kwenye vita na Moscow.

"Rais Biden anaidhinisha kwa dhati kugombea kwa Waziri Mkuu Rutte kuwa Katibu Mkuu ajaye wa NATO," afisa wa Merika alisema. "Waziri Mkuu Rutte ana ufahamu mpana wa umuhimu wa Muungano huu, ni kiogozi wa asili na mjuzi wa kuwasiliana, na uongozi wake utautumikia vyema muungano katika wakati huu muhimu.

Kutegemeana na matokeo ya uchaguzi wa Rais wa Marekani mnamo mwezi Novemba, mkuu ajaye wa NATO huenda akalaazimika kushughulikia muhula wa pili wa Donald Trump, aliekolewa vikali na maafisa wa magharibi mwezi huu kwa kuhoji dhamira yake ya kuwalinda washirika wa NATO ikiwa atachaguliwa tena.

Kiongozi wa Uholanzi aliehudumu kwa muda mrefu zaidi Mark Rutte mwenye umri wa miaka 57, ana uhusiano mzuri na viongozi mbalimbali wa Uingereza na Marekani, akiwemo Trump - wakati wa muhuka wake mrefu madarakani.

Katibu Mkuu wa NATO Jens Stoltenberg, kushoto, na Mark Rutte, Waziri Mkuu wa Uholanzi.Picha: Sem van der Wal/ANP/picture alliance

"Tunapaswa kushirikiana na yeyote alieko madarakani," Rutte alisema siku ya Jumamosi, akiwahimiza viongozi wa Ulaya "kuacha kuomboleza na kulalamika" kuhusu Trump na badala yake wak´jikite juu ya wanachoweza kufanya kwa ajili ya Ukraine.

Ikimuunga mkono Rutte kwa kazi hiyo, Wizara ya Mambo ya Nje ya Uingereza ilisema siku ya Alhamisi kwamba alikuwa mtu anayeheshimika sana kote NATO na mwenye sifa thabiti za ulinzi na usalama, na mtu ambaye atahakikisha inabaki imara na kujiandaa kwa hitaji lolote la kujilinda.

Viongozi wa NATO wanateuliwa kwa makubaliano yanayohitaji kuungwa mkono - au angalau pasina upinzani - kutoka kwa wanachama wake wote 31, kumaanisha uungwaji mkono wa Washington na London ni muhimu lakini hautoshi.

Wanadiplomasia wawili walisema Rutte anaungwa mkono na takriban wanachama 20 wa NATO hadi sasa, lakini mwanadiplomasia mwingine mkuu alionya kuwa makubaliano bado hayajafikiwa na mgombea mwingine bado anaweza kuibuka.

Wanadiplomasia wawili walisema Rutte anaungwa mkono na takriban wanachama 20 wa NATO hadi sasa, lakini mwanadiplomasia mwingine mkuu alionya kuwa makubaliano bado hayajafikiwa na mgombea mwingine bado anaweza kuibuka.

Mkosoaji mkali wa Putin

Wanadiplomasia wameziainisha Hungary na Uturuki zinazoweza kumtilia vigingi lakini hakukuwa na maoni ya haraka kutoka nchi zote mbili juu ya misimamo yake.

Chanzo kutoka serikali ya muungano ya Ujerumani kilisema Berlin pia ilitarajiwa kumuunga mkono Rutte. Lakini Poland haina msimamo bado, msemaji wa wizara ya mambo ya nje alisema.

Mark Rutte akiwa katika mazungumzo na Rais wa Marekani Joe Biden mjini Washington.Picha: Carolyn Kaster/AP/dpa/picture alliance

Chini ya uongozi wa Rutte matumizi ya ulinzi ya Uholanzi yalipunguzwa wakati wa miaka ya mzozo wa kifedha. Tangu uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraine, hata hivyo, Uholanzi imeongeza matumizi kufikia karibu asilimia 2 ya Pato la Taifa mwaka 2024. Rutte kwa muda mrefu amekuwa mkosoaji mkali wa Rais wa Urusi Vladimir Putin.

Rutte bila kutarajiwa alitangaza kuachana na siasa za Uholanzi mwezi Julai, lakini anasalia katika wadhifa wake kama kiongozi wa muda huku mazungumzo ya muungano yakiendelea kufuatia uchaguzi wa Novemba 22. Stoltenberg, waziri mkuu wa zamani wa Norway, amehudumu kama mkuu wa NATO tangu 2014.

Soma pia:Stoltenberg aelezea matumaini ya Sweden kujiunga na NATO

Waziri Mkuu wa Estonia, Kaja Kallas na Waziri wa Mambo ya Nje wa Latvia Krisjanis Karins pia wameonyesha nia ya kugombea nafasi hiyo ya juu ya NATO lakini hawajawasilishwa rasmi kama wagombea, wanadiplomasia wanasema. Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen, ambaye wengine walikuwa wamemtaja kama mrithi anayewezekana, aliondoa uwezekano huo siku ya Alhamisi.

Ikianzishwa mwaka 1949 ili kukabiliana na Umoja wa Kisovieti wakati wa Vita Baridi, NATO ni muungano wa kisiasa na kijeshi wa nchi kutoka Amerika Kaskazini na Ulaya.

Katika kifungu cha 5 cha mkataba wake wa uanzishwaji inatajwa kanuni ya ulinzi wa pamoja - ambayo ni dhana kwamba shambulio dhidi ya mwanachama mmoja linachukuliwa kuwa shambulio dhidi ya wote. Sweden inatazamiwa kuwa mwanachama wa 32 wa muungano huo wa Magharibi.

Chanzo: RTRE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW