1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Ukraine na Urusi zaanza mazungumzo Abu Dhabi

23 Januari 2026

Rais Volodymyr Zelensky amesema mazungumzo ya amani kati ya Ukraine, Marekani na Urusi mjini Abu Dhabi, yatatuama zaidi katika masuala ya kimaeneo haswa kanda ya mashariki mwa Ukraine ya Donbas.

USA Palm Beach 2025 | Trump na Zelensky
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelensky na Rais wa Marekani Donald TrumpPicha: Joe Raedle/AFP/Getty Images

Zelensky amewaeleza waandishi wa habari leo Ijumaa kwamba Donbas itatawala mazungumzo ya leo na kesho yanayofanyika Umoja wa Falme za Kiarabu kati ya maafisa wa Marekani, Ukraine na Urusi. Ameongeza kwa kusema kwamba; "Donbas ni suala muhimu. Litajadiliwa kwa muundo ambao pande tatu zitaona unafaa mjini Abu Dhabi leo na kesho."

Kuelekea mazungumzo ya Abu Dhabi, Urusi imesema kwamba haijaachana na sharti lake kuu linaloitaka Ukraine kuondoka Donbas. Msemaji wa Ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov, ameweka wazi kwamba "msimamo wa Urusi unafahamika wazi kwamba jeshi la Ukraine linapaswa kuondoka kwenye eneo la Donbas," na kuongeza kuwa hilo ni sharti muhimu sana kwa Moscow.

Rais Volodymyr Zelenskyj katika mkutano wa mwaka wa WEFPicha: Fabrice Coffrini/AFP/Getty Images

Pande zote mbili zinadai kwamba hatma ya maeneo ya mashariki mwa Ukraine ni moja ya masuala makuu ambayo bado hayajapatiwa mwafaka katika mchakato wa kutafuta suluhu ya vita ambavyo vimeua makumi kwa maelfu ya watu, kuwahamisha mamilioni, na kuharibu kwa kiasi kikubwa eneo la mashariki mwa Ukraine.

Rais Vladimir Putin amesisitiza mara kdhaa kwamba Moscow inakusudia kuchukua udhibiti kamili wa kanda nzima ya Mashariki mwa Ukraine kwa nguvu, endapo mazungumzo yatashindikana. Kanda ya mashariki ya Donbas inajumuisha sehemu kubwa ya mikoa ya Ukraine ya Donetsk na Luhansk huku Kyiv ikiwa bado inadhibiti kipande cha eneo hilo.

Hapajakuwa na mikutano ya moja kwa moja rasmi kati ya pande mbili zinazopigana kwa miaka kadhaa, ambapo Istanbul ilikuwa eneo la mwisho kufanyika mazungumzo hayo. Hata hivyo, maafisa wa kijeshi wa Urusi na Ukraine wameitumia Abu Dhabi kwa mikutano isiyo rasmi kujadili suala la kubadilishana wafungwa wa kivita. Washington imekuwa ikiongoza jitihada kwa miezi kadhaa kuishawishi Urusi na Ukraine kufikia suluhisho la amani, lakini pande hizo mbili bado zina msimamo unaopingana.

Mashambulizi ya Urusi yameua zaidi ya watu 30 Ukraine

02:10

This browser does not support the video element.

Wakati hayo yakijiri, Umoja wa Ulaya unatarajiwa kukabidhi karibu jenereta 450 za dharura kwa Ukraine kufuatia mashambulizi makubwa ya Urusi kwenye miundombinu ya nishati ya nchi hiyo wakati wa msimu mkali wa baridi. Jenereta hizo zitasaidia kurejesha umeme kwenye hospitali, makazi ya dharura na huduma muhimu.

Ukraine imekuwa ikikumbwa na baridi kali tangu mwanzoni mwa Januari, huku hali ikizidi kuwa mbaya zaidi kutokana na mashambulizi ya Urusi dhidi ya miundombinu ya nchi hiyo, ambayo yamewaacha mamilioni bila umeme. Poland pia itapeleka mamia ya jenereta kusaidia raia wa Ukraine wanaoteseka na baridi kali.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW