1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani, Ulaya waionya Sudan kuhusu uteuzi mpya

5 Januari 2022

Marekani na Umoja wa Ulaya wameionya Sudan juu ya uteuzi wa waziri mkuu mpya baada ya kiongozi wa kiraia Abdallah Hamdok kujiuzulu katikati ya maandamano ya kuupinga utawala wa kijeshi. 

Sudan politische Krise | Proteste in Khartum
Picha: AFP/Getty Images

Marekani, Uingereza, Norway pamoja na Umoja wa Ulaya kwa pamoja wamesema hawatamuunga mkono waziri mkuu atakayeteuliwa, iwapo wadau wengi wa kiraia hawatahusishwa, imesema sehemu ya taarifa hiyo iliyotolewa na wizara ya mambo ya nje ya Marekani.

Taarifa hiyo ya pamoja pia imetoa mwito wa kuendelea kwa maandalizi ya uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwaka 2023 chini ya makubaliano ya kipindi cha mpito, lakini pia kuimarishwa kwa mfumo wa huru wa mahakama na bunge, huku ikionya hatua ya upande mmoja ya kuteua waziri mkuu mpya na baraza la mawaziri inaweza kudhoofisha uaminifu wa taasisi hizo.

Sehemu ya taarifa hiyo aidha imewaomba wadau kwenye mvutano huo kujizatiti ili kuhakikisha mazungumzo yatakayoongozwa na Sudan na kuratibiwa kimataifa yanafanyika mara moja, ili hatimaye waweze kushughulikia masuala ya sasa na mengineyo ya mpito.

Mataifa hayo manne yenye nguvu kubwa kiuchumi ulimwenguni aidha yamesema bado yanaamini katika mabadilishano ya madaraka kwa njia ya demokrasia nchini Sudan, lakini kwa upande mwingine yakalionya jeshi iwapo litashindwa kuchukua hatua za kusonga mbele.

Aliyekuwa waziri mkuu wa Sudan, Abdallah Hamdok alijiuzulu wiki sita baada ya kurejea kwenye wadhifa huo.Picha: Mohamed Khidir/Xinhua/Imago Images

Aliyekuwa waziri mkuu Abdallah Hamdok alitangaza kujiuzulu Jumapili iliyopita.

Mataifa ya magharibi yahofia hatua za kijeshi kwa waandamanaji.

Mataifa makubwa ya magharibi yalimkaribisha waziri mkuu huyo, mwanauchumi na afisa wa zamani wa Umoja wa Mataifa, lakini wachambuzi walimchukulia kama ambaye hakuwa na umuhimu wowote na hasa baada ya serikali yake kupunduliwa kwenye mapinduzi ya kijeshi ya Oktoba mwaka jana, na baadae kurejea kwenye nafasi yake.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price alisema taifa hilo bado linaamini katika makubaliano ya mwaka 2019 yaliyofikiwa kati ya waandamanaji na jeshi lililomuondoa madarakani aliyekuwa kiongozi wa taifa hilo Omar al-Bashir.

Kwenye taarifa hiyo, mataifa hayo pia yameelezea wasiwasi wao kuhusiana na hatua za jeshi dhidi ya waandamanaji yakisema raia wana haki ya kuandamana.

Jana Jumanne, vikosi vya usalama vilitumia gesi ya machozi kuwatawanya waandamanaji hao wanaoupinga utawala wa kijeshi, lakini pia taarifa za karibuni za vifo vya waandamanaji kote katika mji mkuu wa Sudan, Khartoum pamoja na majiji ya jirani, hii ikiwa ni kulingana na shuhuda aliyezungumza na shirika la habari la Reuters.

Soma Zaidi: Sudan: Vikosi vya usalama vyatumia gesi ya kutoa machozi dhidi ya waandamanaji

Mashirika: RTRE/AFPE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW