1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Urusi haina nia ya kuvimaliza vita Ukraine

13 Novemba 2025

Mawaziri wa mambo ya kigeni wa kundi la nchi saba zilizoendelea kiviwanda duniani G7 wamejadiliana jinsi ya kuishinikiza Urusi katika vita vyake nchini Ukraine.

Mawaziri wa nchi za kigeni wa nchi za G7 wakiwa Niagara, canada
Mawaziri wa nchi za kigeni wa nchi za G7 wakiwa Niagara, canadaPicha: Nick Iwanyshyn/AP Photo/picture alliance

Haya yanafanyika wakati ambapo kuna mashaka iwapo Moscow inataka kuvisitisha vita hivyo.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Marco Rubio ni miongonimwa waliokuwa katika eneo la Niagara huko Canada katika mkutano huo wa mawaziri wa mambo ya nje wa G7 ambao pia ulihudhuriwa na waziri wa mambo ya kigeni wa Ukraine, Andrii Sybiha.

Sybiha amewataka washirika wa Ukraine kuimarisha uwezo wake wa kutumia makombora ya masafa marefu na kuiimarisha pia sekta yake ya nishati wakati ambapo nchi hiyo inaingia katika msimu wa baridi kwa mara nyengine ikiwa vitani.

Urusi inalitaka eneo zima la Donetsk

Mara baada ya mkutano huo Rubio alisema Marekani haioni nia ya Urusi ya kutaka kuusitisha mzozo huo.

"Tunakwenda na tunachokiona na nafikiri Warusi wamesema wazi kile wanachokitaka na ni kwamba wanaitaka Donetsk nzima na bila shaka Waukraine hawatolikubali hilo. Kwa hiyo tunachokiona sasa ni kwamba wanaendelea kurusha makombora ya masafa marefu ndani ya Ukraine, kwa ajili ya kuiharibu gridi ya umeme ya taifa na mambo kama hayo," alisema Rubio.

Waziri wa mambo ya nje wa Marekani marco Rubio (kulia) akiwa na mwenyeji wake wa Canada Anita Anand (kushoto)Picha: Nick Iwanyshyn/ZUMA/IMAGO

Mkuu wa sera za kigeni wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas pembezoni mwa mkutano huo amewaambia waandishi wa habari kuwa mazungumzo kuhusu Ukraine kwa sasa yanajikita tu kwenye kuiwekea shinikizo zaidi Urusi.

Lakini waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi Sergei Lavrov katika mahojiano yaliyochapishwa usiku wa kuamkia leo, amesema anatarajia kuwa Marekani haitochukua hatua zitakazosababisha kuongezeka kwa mzozo huo wa Ukraine.

Urusi yatanua juhudi za kuyateka maeneo zaidi Ukraine

Lavrov amesema Rais wa Marekani Donald Trump kwa muda amekuwa akitaka mazungumzo na Urusi ili apate uelewa kamili wa inachokitaka Urusi kwa Ukraine, na kwamba ameonesha nia ya kupata suluhisho la amani la kudumu.

Waziri wa mambo ya kigeni wa Urusi sergei LavrovPicha: Shamil Zhumatov/REUTERS

Lavrov ameyasema haya wakati ambapo kamanda mkuu wa jeshi la Ukraine Jenerali Oleksandr Syrskyi amesema Urusi imeyateka maeneo matatu ya makaazi kusini mwa Zaporizhzhia, wakati ambapo wanatanua juhudi zao za kuyateka maeneo zaidi ya Ukraine.

Jenerali Syrskyi amesema ukungu mzito ndio uliosababisha wanajeshi wa Urusi kuyavamia maeneo ya majeshi ya Ukraine huko Zaporizhzhia na akaongeza kuwa wanajeshi wake wanapambana ili kuwarejesha nyuma Warusi.

Kamanda huyo mkuu lakini amesema mapambano makali bado yako katika eneo lililovamiwa la Pokrovsk mashariki mwa eneo la Donetsk, ambako karibu nusu ya mapambano yote ya mstari wa mbele yalifanyika katika kipindi cha saa 24 zilizopita.

Vyanzo: Reuters/APE

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW