Marekani: Urusi ilifanya uhalifu wa kivita Kherson
22 Novemba 2022Hatua hii inaonyesha kwamba huenda maafisa wakuu katika serikali ya Urusi walihusika katika uhalifu wa kivita. Haya yanafanyika wakati ambapo Ukraine inasema imegundua maeneo 4 yaliyokuwa yanatumiwa na Urusi kuwatesa Waukraine katika eneo lililokombolewa hivi majuzi la Kherson.
Akizungumza na waandishi wa habari mjini Washington, balozi wa Marekani kuhusiana na Sheria ya Uhalifu Duniani Beth Van Schaack amesema kuna ushahidi mkubwa kwamba vitendo vya mateso vya Urusi nchini Ukraine havikutekelezwa kwa kushtukiza tu.
Van Schaack amesema kuna ushahidi kwamba uvamizi wa Urusi nchini Ukraine umeandamana na vitendo vya uhalifu wa kivita katika kila eneo ambalo majeshi ya Urusi yalitumwa.
Maeneo 4 ya mateso yagunduliwa Kherson
Balozi huyo anasema ushahidi kutoka maeneo yaliyokombolewa unaonyesha raia na wafungwa wa kivita walishambuliwa na kuteswa kwa kusudi. Waukraine wakiwemo watoto waliondolewa na kupelekwa Urusi kwa lazima na zaidi ya hayo kulikwua na mauaji na udhalilishaji wa kingono.
Nayo afisi ya mwendesha mashtaka mkuu wa Ukraine imetoa taarifa iliyosema kwamba imegundua maeneo 4 yaliyotumiwa na Urusi kuwazuia na kuwatesa watu huko Kherson. Afisi hiyo ya mwendesha mashtaka inasema imegundua maeneo hayo baada ya kufanya uchunguzi kwa ushirikiano na maafisa wa polisi na wataalam.
Taarifa hiyo imesema walipata sime na kifaa kilichotumiwa na majeshi ya Urusi kuwatesa watu kwa kutumia umeme. Mamlaka za Urusi pia ziliacha nyaraka zilizoonyesha uongozi wa maeneo hayo ya mateso. Mkaazi mmoja wa Kherson ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kuwa aliteswa kwa wiki kadhaa katika mojawapo ya maeneo hayo.
NATO iitambue Urusi kama taifa la kigaidi
Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskiy kwa mara nyengine ameitaka jumuiya ya kujihami ya NATO na marafiki zake kuitambua Urusi kama taifa la kigaidi.
"Natoa wito kwa jumuiya ya NATO kuchukua hatua madhubuti kutekeleza mpango wa amani wa Ukraine unaoweza kuhakikisha amani na haki kwa Ukraine na jamii nzima ya Ulaya na Atlantiki. Natoa wito pia kwa mabunge yote ya nchi wanachama wa jumuiya ya NATO kuchukua uamuzi wa kuitambua Urusi kama taifa la kigaidi. Naamini kwamba pole pole tutafika hapa, hivi ndivyo Urusi itakavyoonekana duniani," alisema Zelenskiy.
Hayo yakiarifiwa mamlaka nchini Ukraine zimeanza kuwaondoa raia kutoka maeneo yaliyokombolewa hivi majuzi ya Kherson na Mykolaiv kwa hofu kwamba ukosefu wa umeme na maji kutokana na mashambulizi ya Urusi, ni jambo litakalofanya hali ya maisha kuwa ngumu zaidi katika kipindi hiki cha majira ya baridi.
Naibu waziri mkuu wa Ukraine Iryna Vreshchuk amesema serikali itawapa raia usafiri, makazi na matibabu huku watakaopewa kipau mbele wakiwa kina mama wenye watoto, wagonjwa na wazee.
Chanzo: AP/AFP