1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani: Wademocrat kuendelea kudhibiti baraza la seneti

13 Novemba 2022

Chama cha rais wa Marekani Democratic kimeendelea kudhibiti Baraza la Seneti la nchi hiyo baada ya kupata ushindi muhimu katika jimbo la Nevada.

USA , Nevada | Catherine Cortez Masto
Picha: Anna Moneymaker/Getty Images

Ushindi huo umekaidi tabiri za awali kwamba kungekuwa na ‘wimbi la ushindi' wa chama cha Republican.

Seneta Catherine Cortez Masto wa chama cha Democratic aliyekuwa akikitetea kiti hicho alikuwa njiani kuhifadhi kiti hicho baada ya kumshinda mshindani wake wa Republican Adam Laxalt kwa ushindi mwembamba katika uchaguzi huo wa katikati ya muhula.

Jumamosi usiku, mashirika ya Habari ya Marekani NBC na CNN yalimpigia upatu Masto kushinda.

Biden kukutana na Xi Jinping

Rais Joe Biden aliyesherehekea ushindi huo akiwa katika ziara kwenye mji mkuu wa Cambodia Phnom Penh, alisema amefurahishwa sana. Biden anahudhuria mkutano wa kilele wa kiushirikiano wa Jumuiya ya mataifa ya Kusini na Mashariki mwa bara ASIA, ASEAN.

Rais wa Marekani Joe Biden.Picha: Alex Brandon/AP Photo/picture alliance

"Ninahisi vizuri, na ninatazamia hali hiyo katika miaka kadhaa ijayo,” Biden aliwaambia waandishi wa Habari hayo baada ya kumalizika kwa zoezi lililochukua muda mrefu la kuhesabu kura za jimbo la Nevada.

Kuhesabiwa kwa kura za uchaguzi uliofanyika Jumanne, kulikawia kumalizika katika jimbo la Nevada kwa sababu ushindani mkali baina ya wagombea na vilevile kwa sababu ya sheria za uchaguzi.

Ushindi huo umebashiriwa kukiweka chama cha Democratic mbele kikiwa na viti 50 bungeni dhidi ya Warepublican wanaobashiriwa kupata viti 49. Hivyo kuwapa Wademocrat nafasi ya kurefusha udhibiti wa baraza hilo kwa miaka mingine miwili.

Marekani: Matokeo ya uchaguzi wa katikati ya muhula bado yasubiriwa

Hata kama Warepublican watashinda kiti ambacho kimesalia cha jimbo la Georgia, Wademocrat bado watashikilia udhibiti kwa sababu naibu rais Kamala Harris ataweza kupiga kura itakayoupa upande wao wingi wa viti.

Adam Laxalt (kushoto) Mrepublican aliyekuwa akiwania useneta jimbo la Nevada na kulia na rais wa zamani wa Marekani Donald Trump wakati wa kampeni za mwisho kuelekea uchaguzi wa katikati ya muhula.Picha: Peter Dasilva/EPA-EFE

Katika jimbo la Gergia kutakuwa na duru ya pili ya uchaguzi baada ya washindani wawili, Seneta Raphael Warnock wa Democratic na mshindani wake mwanasoka wa zamani Herschel Warnock anayeungwa mkono na rais wa zamani Donald Trump kushindwa kupata Zaidi ya 50% kila mmoja. Hayo ni kulingana na tabiri za mashirika.

Mnamo Jumanne, wapiga kura nchini Marekani walielekea vituoni kuamua upande gani utakuwa na wingi katika baraza la wawakilishi na katika baraza la Seneti. Uamuzi unaobaini nini haswa rais Biden anaweza kufanya kisiasa katika miaka yake miwili iliyosalia kabla ya uchaguzi mkuu wa urais mwaka 2024, na ambayo rais wa zamani Donald Trump anatarajiwa kuwania.

Pamoja na viti vyote vya wawakilishi, viti 35 kati ya jumla ya viti 100 vya useneti vilivyowaniwa mwaka huu. Kabla ya uchaguzi Baraza la Senati lilikuwa limegawika kwa njia sare. Warepublican wana viti 50 vilevile Wademocrat wana viti 50, huku kura ya makamu wa rais Harris ikiwa ya kuvunja sare hiyo.

Viti kadhaa vya ugavana pia vilikuwa vikishindaniwa, hali kadhalika ofisi nyingine muhumi za kisiasa. Ilipofikia Jumatano wiki iliyopita, ilikuwa bayana kwamba majimbo ya Arizona, Georgia na Nevada ndiyo yangebaini ni upande upi utadhibiti seneti.Picha: CARLOS BARRIA/REUTERS

Mnamo Ijumaa mashirika ya Habari ya Marekani yalisema seneta wa Arizona Mark Kelly alikihifadhi kiti hicho.

Hata hivyo Warepublican walikuwa mbioni kuhifadhi wingi wa viti katika baraza la wawakilishi lenye jumla ya viti 435 japo kwa idadi ndogo tofauti na ilivyotabioriwa na wachambuzi.

Wademocrat wamebashiriwa kupata jumla ya viti 204 huku Warepulican wakiongoza kwa viti 211. Pande zote bado hazijafikiwa idadi kamili ya viti 218 inayohitajika kupata wingi kamili bungeni.

Ikiwa Wademokrat watapoteza wingi bungeni, Warepublican wataweza kuzuia misuada ya Warepublican hadi uchaguzi mwingine wa urais Novemba 2024.

(DPAE)