Marekani watetea ubingwa wao
8 Julai 2019Kwa ushindi huo Marekani pia wamefanikiwa kulitetea taji lao walilolishinda katika makala iliyopita ya mashindano hayo ya kina dada.
Mshambuliaji wao mahiri Megan Rapinoe ndiye aliyefunga goli la kwanza mnamo kipindi cha pili baada ya kupachika wavuni mkwaju wa penalti dakika ilipokuwa sitini na moja.
Bao la pili lilitiwa wavuni na Rose Lavelle aqliyeachia mkwaju mkali kutoka yadi kumi na nane.
Rapinoe ashinda tuzo ya mfungaji bora na mchezaji bora wa Kombe la Dunia
Rapinoe ambaye ndiye nahodha wa Marekani ana umri wa miaka 34 na kwa kufunga jana aliingia katika vitabu vya kumbukumbu kwa kuwa mchezaji mwenye umri mkubwa zaidi kuwahi kufunga katika fainali.
Goli hilo la jana lilimfanya aweze kuishinda zawadi ya mfungaji bora na pia akatunukiwa tuzo ya mpira wa dhahabu kama mchezaji bora wa Kombe hilo la Dunia.
Rais Donald Trump alikuwa miongoni mwa waliowapongeza kina dada hao kwa ushindi huo.
"Naipongeza timu ya kina dada ya Marekani kwa ushindi, ilikuwa mechi nzuri sana na niliitazama kidogo. Ni wachezaji wazuri na ni fahari kubwa wao kuishindia Marekani taji hilo kwa mara ya nne," alisema Trump.
Lakini baadhi ya wachezaji katika timu hiyo wakiongozwa na nahodha wao Rapinoe wamesema watasusia mwaliko wa Trump katika ikulu ya White House iwapo atawaalika kutokana na kauli zake za kibaguzi.