1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
JamiiMarekani

Marekani: Wazazi wahofia kujadili ufyatuaji risasi mashuleni

30 Machi 2023

Marekani imekuwa ikishuhudia matukio kadhaa ya ufyatuaji risasi mashuleni. Wazazi nchini humo wanakabiliwa na hofu juu ya jinsi watakavyoweza kujadiliana na watoto wao kuhusu matukio hayo bila hata hivyo kuwatisha.

USA Nashville | Schießerei an Covenant School
Picha: Kevin Wurm/REUTERS

Wakati Elizabeth Barese alipokwenda siku ya Jumatatu kumchukua shuleni mtoto wake wa kiume mwenye umri wa miaka 11, alifahamu wazi kwamba alipaswa kumueleza mara moja kuhusu tukio la ufyatuaji risasi lililotokea siku hiyo hiyo katika shule jirani na nyumba yao huko Nashville.

Mzazi huyo mwenye umri wa miaka 47 ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, alilazimika kuzungumza na mwanaye kwa sababu wanaishi karibu na eneo la tukio na kulikuwa na idadi  kubwa ya polisi.   

Shule ya The Convenant, Nashville kulikotokea mauaji hayo.Picha: John Amis/AP

Akiwa amesimama mbele ya misalaba iliyojengwa nje ya lango la Shule ya "The Covenant" likiwa na majina ya wahanga sita, watatu kati yao wakiwa watoto wadogo, Barese alisema hakika si mada ambayo mzazi yeyote angelipenda kuzungumza na watoto wake, kwa maana ni lazima utafute usawa mzuri wa kuwa mwaminifu kwa watoto bila hata hivyo kuwatisha. 

Mtanziko huo unawakabili wazazi wengi nchini Marekani kufuatia tukio jingine la ufyetuaji risasi katika shule ambalo limeitikisa nchi hiyo, na kuwaacha wazazi hao wakihitaji kuwafariji watoto wao wakati wote huku na wenyewe wakigubikwa na huzuni na woga.

Soma pia:Watu wanane wauawa kwa kupigwa risasi Marekani   

Mashambulizi ya kutumia bunduki ni jambo linaloshuhudiwa mara kwa mara nchini Marekani, nchi yenye watu wapatao milioni 330 ambao wana zaidi ya bunduki milioni 400. Shule hazijaepuka matukio hayo, na mashambulio kwenye taasisi za elimu yamekuwa yakiripotiwa mara kadhaa. 

Kulingana na takwimu iliyokusanywa na jarida la The Washington Post, tangu mauaji ya Shule ya Upili ya Columbine mnamo mwaka 1999, kumekuwa na matukio 376 ya ufyatuaji risasi mashuleni kote nchini Marekani,  ambapo watu 199 waliuawa na wengine 424 walijeruhiwa. Kwa ujumla, data hizo zimebaini kuwa zaidi ya wanafunzi 348,000 walikabiliwa na vurugu za bunduki mashuleni mwao.

Mazoezi ya bunduki mashuleni yashamiri kutokana na hofu

Wanafunzi wa Shule ya The Convenant wakionesha mshikamano baada ya tukio la mauaji shuleni kwao.Picha: Jonathan Mattise/AP/picture alliance

Kwa wazazi wengi wa Marekani, idadi ya matukio hayo inayoongezeka inazidisha wasiwasi kuwa huenda shule ya watoto wao ikawa ndiyo inayofuata. Utafiti wa Kituo cha Pew wa mwaka 2022 ulibaini kuwa takriban theluthi moja ya wazazi wa watoto walio na umri wa kwenda shule wamesema kuwa na wasiwasi mkubwa. 

Baada ya tukio la ufyatuaji risasi katika shule ya msingi huko Uvalde, Texas na kusababisha vifo vya watu 21, Barese alisema aliandika ujumbe kwenye mtandao wa kijamii akisema hajui ni lini tukio jingine litatokea lakini ana uhakika ni lazima litatokea ila anatumai isiwe katika mji wake wa Nashville.

Soma pia: Trump kuwapa bunduki waalimu

Xsavier Cleary, ambaye anaishi karibu kilomita 50 kutoka shule ya msingi ya Covenant, alikuja kutoa salamu za rambirambi huku usalama wa watoto wake ukiwa akilini mwake. Kwa sasa anauliza ikiwa watoto wao bado wako salama mashuleni.

Siku ya Jumatatu Cleary, alisema watoto wake, wenye umri wa kuanzia miaka mitatu hadi 22, hawakuweza kuepuka mazungumzo ya ufyatuaji risasi huo, ambapo mtu mwenye umri wa miaka 28 aliyekuwa na silaha alivamia shule ndogo ya Kikristo ya kibinafsi na kuwaua watu sita wakiwemo wafanyakazi watatu na wanafunzi watatu.

Picha: AP

Anasema hakutarajia kuwa na mazungumzo kama hayo na watoto wake ambao wako shule ya msingi ili kuwaambia nini cha kufanya na kujiandaa, ikiwa kitu kama hicho kitatokea.

Mazoezi ya kutumia bunduki yameongezeka katika shule nchini Marekani, kama alivyoshuhudia Barese katika shule ya mtoto wake. Alisema kwa hisia kuwa hali hiyo ilimfanya atokwe na machozi.

Baada ya ufyatuaji risasi katika Shule ya Msingi ya Sandy Hook mwaka 2012, ambapo watoto 20 na watu wazima sita waliuawa, shule ya awali ya binti yake wa umri wa miaka mitatu wakati huo ilianza mazoezi ya kutumia bunduki, jambo ambalo Barese alisema lilimkera sana.

Mada inayohusiana: 

Kijana aua watoto Marekani

01:43

This browser does not support the video element.

Lakini Barese, ambaye ameishi huko Tennessee kwa miaka 18, amesema anatambua umuhimu wa ushauri ambao shule ya mtoto wake imekuwa ikitoa kuhusu jinsi ya kukabiliana na tukio la siku ya Jumatatu.

Kwa miaka mingi, wanasaikolojia wa Marekani wamekuwa wakitoa nyenzo muhimu ili kuwasaidia wazazi jinsi ya kushughulikia mijadala kama hiyo.  Chama cha Kitaifa cha Wanasaikolojia wa Mashuleni (NASP) huweka vidokezo mtandaoni kwa ajili ya wazazi na walimu kuhusu jinsi ya kuzungumza na watoto kuhusu matukio hayo ya vurugu, ikiwa ni pamoja na yale yanayotokea mashuleni.

(Chanzo: AFPE)

 

    

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW