1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaadhimisha mwaka wa mauaji ya George Floyd

25 Mei 2021

Marekani lnaadhimisha kumbukumbu ya mwaka mmoja tangu kutokea mauaji ya George Floyd, Mmarekani mweusi aliyekufa mikononi mwa polisi mzungu. Rais Joe Biden ameialika familia ya Floyd katika ikulu ya Marekani.

TABLEAU | USA Prozess George Floyd  | Derek Chauvin Demonstration
Picha: NICHOLAS PFOSI/REUTERS

Bintiye Floyd Gianna, mamake, dada na kaka zake watakuwa miongoni mwa wale watakaohudhuria mazungumzo ya faragha na Biden katika ikulu ya White House, mjini Washington. Msemaji wa ikulu ya Marekani, Jen Psaki, amewaambia wanahabari kwamba ujasiri na neema ya familia ya Floyd na haswa binti yake Gianna, umemgusa rais, na kwamba ana hamu ya kusikiliza mitazamo yao.

Huku hayo yakijiri, hapo jana wakati wa mkesha wa maadhimisho ya mwakammoja tangu kuuawa kwa Floyd, mazungumzo ya jopo lililoandaliwa na wakfu wa George Floyd ulioanzishwa na dada yake Bridgett yalioongozwa na mwanaharakati wa Black Lives Matter DeRay Mckesson katika mji wa Minneapolisi alikouawa Floyd mwaka jana, wazazi na ndugu za Wamarekani Weusi waliouawa na polisi, waliwahimiza watu kujiunga nao katika kufuatilia mabadiliko ya kisheria ambayo walisema yanaweza kupunguza vifo kama hivyo katika siku zijazo.

Wito kutoka kwa jamaa za familia za waathiriwa

Maandamano ya kutaka haki kwa mauaji ya George FloydPicha: OCTAVIO JONES/REUTERS

Jamaa za familia za Eric Garner, Trayvon Martin, Daunte Wright na Wamarekani wengine weusi waliouawa mikononi mwa polisi, walikusanyika kuzungumza kuhusu hali ya sera nchini Marekani na ubaguzi wa rangi katika mashambulizi ya polisi. Familia hizo pia zilizungumzia jukumu la wabunge katika kufanya mabadiliko ya kuwajumuisha polisi na jinsi jamaa wanawavyoweza kuzisaidia familia za wale waliouawa na polisi.

Kifo cha Floyd kilichotokea Mei 25 mwaka jana baada ya kugandamiziwa goti kwenye shingo kwa zaidi ya dakika nane na polisi mzungu Derek Chauvin anayesubiri hukumu yake, kilionekana kama nyakati ya giza katika harakati za muda mrefu za Marekani za kuumaliza ubaguzi wa rangi.

Mchakato ulioanzishwa na Biden

 Wakati wa uamuzi wa mahakama dhidi ya Chauvin mwezi Aprili mwaka huu atakayehukumiwa mwezi ujao, Biden alitafuta kuanzisha mchakato wa kisiasa kwa kulihimiza bunge kupitisha muswada wa marekebisho katika idara ya polisi kabla ya maadhimisho ya mwaka mmoja ya kifo cha Floyd.

Biden alisema kuwa Wamarekani lazima wakabiliane na ubaguzi wa rangi uliodhihirishwa na kifo cha Floyd. Hata hivyo, muda huo wa mwisho umewadia huku bunge hilo likiwa limepitisha tu muswada wa sheria uliopewa jina la George Floyd, huku baraza la seneti likiendelea kuvutana kuhusu maelezo muhimu.