1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaahidi msaada mpya wa dola milioni 60 kwa Ukraine

2 Septemba 2021

Rais wa Marekani Joe Biden ametumia mkutano wake wa kwanza na kiongozi wa kigeni tangu kukamilika kwa vita nchini Afghanistan kutuma ujumbe kwamba Marekani, inadhamiria kuwa mshirika muhimu na wa kuaminika kwa Ukraine.

USA I Joe Biden und  Volodymyr Zelenskyy im Oval Office
Picha: Doug Mills/CNP/picture alliance

Rais Joe Biden alikuwa mwenyeji wa Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy, na kumuhakikishia kwamba utawala wake unaiunga mkono nchi hiyo ya Mashariki mwa Ulaya.

"Tunaposherehekea maadhimisho ya miaka 30 ya uhuru wa Ukraine, ushirikiano kati ya mataifa yetu utazidi kuwa na nguvu na kuimarika hata kuliko ilivyokuwa"

Biden ameelezea wasiwasi wake juu ya hatua ya uchokozi ya Urusi katika eneo la mashariki mwa Ukraine ambapo wapiganaji wanaotaka kujitenga wanaoungwa mkono na Urusi wamekuwa wakipambana na wanajeshi wa serikali ya Ukraine.

Soma zaidi: Merkel, Zelensky waujadili mradi wa gesi wa Nord Stream 2

Rais huyo wa Marekani akitetea uamuzi wake wa kumaliza vita vya miaka 20 nchini Afghanistan, amesema hatua hiyo itaisaidia Marekani kushughulikia masuala mengine kama vile kupambana na vitendo viovu kutoka kwa maadui wake, Urusi na China.

Biden aelezea wasiwasi wake juu ya hatua ya uchokozi ya Urusi katika eneo la mashariki mwa Ukraine

Picha: Eric Baradat/Pavel Golovkin/AFP

Kiongozi huyo wa Ukraine amewasili Ikulu ya White House akinuia kupata usaidizi wa kijeshi kutoka Marekani na pia anatafuta uungwaji mkono wa nchi yake kupata uwanachama katika jumuiya ya ushirika wa kijeshi ya NATO.

Utawala wa Biden umesema uko tayari kutoa hadi dola milioni 60 ya msaada wa kijeshi kwa Ukraine. Biden amesema msaada huo ni muhimu kwa sababu ya kuongezeka operesheni za jeshi la Urusi katika mpaka wake pamoja na kuisadia Ukraine kukabiliana na aina nyengine za uchokozi.

Soma zaidi: Makubaliano ya Nord Stream 2 yazua hofu ya uchokozi wa Urusi mashariki mwa Ulaya

Katika mazungumzo yao ya faragha, Zelenksyy na Biden pia walijadiliana juu ya uamuzi wa Washington wa kupinga ujenzi wa mradi wa bomba la gesi wa Nord Stream 2. Mradi huo pia unapingwa na Ukraine na Poland, huku Zelenksyy akiuelezea kama silaha ya kisiasa ya Urusi.

Mkutano huo awali uliahirishwa kwa siku mbili wakati Biden na timu yake ya usalama ilipokuwa inashughulikia suala la kuondoa wanajeshi wa Marekani nchini Afghanistan. Wanajeshi wa mwisho wa Marekani waliondoka Afghanistan mnamo siku ya Jumatatu.

Hata hivyo, Biden anakabiliwa na ukosoaji mkubwa kwamba operesheni hiyo haikuandaliwa vizuri na kuionyesha Marekani kama mshirika wa kimataifa asiyeaminika.