1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaAsia

Marekani yaanza kuondosha wanajeshi Afghanistan

1 Mei 2021

Marekani imeanza awamu ya mwisho ya kuwaondowa wanajeshi wake nchini Afghanistan, huku mashambulizi mapya yakiripotiwa licha ya ulinzi kuimarishwa kwenye maeneo kadhaa ya taifa hilo la Asia. 

Nato Truppen verlassen Afghanistan
Picha: Vyacheslav Oseledkov/AFP/Getty Images

Wanajeshi wawili wa Afghanistan waliuawa na wengine 18 kujeruhiwa siku ya Jumamosi (Mei Mosi), baada ya mripuko kutokea ndani ya kambi ya jeshi la anga la Bagram iliyo kwenye jimbo la kaskazini la Parwan.

Hakuna kundi lililodai kuhusika na mashambulizi hayo. 

Naibu mkuu wa polisi wa jimbo hilo, Abdul Wasay Rahimi aliliambia shirika la habari la Ujerumani, dpa, kwamba bomu lililotegwa kwenye dari liliripuka ndani ya msikiti ulio kwenye kambi hiyo wakati wa sala ya taraweh. 

Kwa mujibu wa Rahimi, kituo hicho cha kijeshi kipo mita chache kutoka vilipo vikosi vya kimataifa, wakiwemo wanajeshi wa Marekani na wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO ambao walianza rasmi kuondoka nchini Afghanistan siku ya Jumamosi. 

Rais Joe Biden aliiweka tarehe Mosi Mei kuwa mwanzo rasmi wa kujiondowa kwa wanajeshi waliobakia nchini Afghanistan, lakini mchakato huo hautakamilika hadi tarehe 11 Septemba 2021, msimamo uliopingwa vikali na kundi la Taliban. 

Kwa mujibu wa makubaliano kati ya utawala wa aliyekuwa rais wa Marekani, Donald Trump, na kundi la Taliban, hiyo ilikuwa ni tarehe ya kukamilisha uondokaji wa wanajeshi hao. Marekani ilikuwa imebakisha kati ya wanajeshi 2,500 hadi 3,500 huku NATO ikiwa na wanajeshi 7,000.

Ulinzi waimarishwa Kabul

Marekani yaanza kuondowa wanajeshi wake AfghanistanPicha: Javed Tanveer/AFP/Getty Images

Katika mji mkuu, Kabul, ambako bado idadi kubwa ya wanajeshi wa Marekani wanaendelea kusalia, ulinzi umeimarishwa na kumewekwa vizuizi kadhaa vya barabarani.

Marekani inakisiwa kutumia zaidi ya dola trilioni mbili ndani ya kipindi cha miongo miwili ya operesheni ya kijeshi, kwa mujibu wa mradi wa Costs of War unaosimamiwa na Chuo Kikuu cha Brown, ambao unaorodhesha gharama za kampeni ya kijeshi ya Marekani.

Maafisa wa wizara ya ulinzi ya Marekani pamoja na wanadiplomasia waliliambia shirika la habari la AP kwamba hatua za sasa za kuondowa wanajeshi zinahusisha vituo vidogo vya kijeshi. 

Tangu Biden kutangaza uamuzi wa kuondowa wanajeshi katikati ya Aprili, ni wanajeshi 60 tu walioondoka nchini Afghanistan.

Marekani na washirika wake wa NATO waliivamia Afghanistan tarehe 7 Oktoba 2001 kwa madai ya kuwasaka wapiganaji wa al-Qaida waliohusika na mashambulizi ya kigaidi ya tarehe 11 Septemba mwaka huo, waliokuwa wakipewa hifadhi na utawala wa wakati huo wa Afghanistan chini ya kundi la Taliban.

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW