1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Marekani yaanza rasmi mchakato kujitoa mkataba wa Mazingira

Sekione Kitojo
5 Novemba 2019

Marekani imeanza rasmi mchakato kujitoa kutoka makubaliano ya mazingira, waziri wa mambo ya kigeni wa Marekani Mike Pompeo alitangaza, siku ya kwanza ambayo inawezekana kwa Washington kuchukua hatua  hiyo kisheria.

Mike Pompeo
Picha: picture-alliance/dpa/AP/M. Altaffer

Rais wa  Marekani Donald Trump  alikuwa  mpinzani  mkubwa  wa makubaliano  hayo  wakati  alipokuwa  anawania  kiti  cha  urais, na utawala  wake  umekuwa  ukifanya  kila  unaloliweza kubadilisha sheria  za  mazingira, ukisema zinazuwia  biashara  na  kutoa  kwa nchi  nyingine  nguvu  ya  ushindani.

Rais Trump akizungumza juu ya jukumu la Marekani katika mkataba wa Paris wa mazingira , Juni mosi ,2017 mjini WashingtonPicha: picture-alliance/AP Photo/P. M. Monsivais

Pompeo alielezea  kuhusu kile  alichokiita "mzigo usio wa  haki wa kiuchumi uliowekwa  kwa  wafanyakazi wa  Marekani, biashara, na walipa  kodi, kwa  ahadi za Marekani  zilizotolewa  chini  ya makubaliano  hayo," wakati  akitangaza  kujitoa  huko. Amesema ,"mfano bora  na  wenye  uhalisia" utapendekezwa  na  Marekani kupinga  makubaliano  hayo  ya  dunia.

Mkubaliano  ya  mwaka  2015 yalitiwa  saini  na  karibu  nchi  zote, na  kuuweka  utawala  wa  Trump  dhidi  ya  karibu  washirika  wake wote  pamoja  na  washindani  wake  wakuu  kuhusiana  na  suala  la mabadiliko  ya  tabia  nchi. Trump  binafsi  ni  mtu  mwenye  shaka na  mabadiliko  ya  tabia  nchi.

Umoja wa  mataifa waarifiwa

Utawala  wa  Trump rasmi uliuarifu  Umoja  wa  mataifa  hatua  yake hiyo  ya  kujitoa  jana  Jumatatu, ukianza  mchakato  wa  mwaka mmoja  ambao  utakamilika  siku  moja  baada  ya  uchaguzi  wa  rais wa  Marekani  mwaka  2020.

Waandamanaji mjini Washington wakipinga kujitoa Marekani kutoka mkataba wa mazingira wa Paris.Picha: Picture alliance/AP Images/S. Walsh

Msemaji  wa  Umoja  wa  mataifa  alilithibitishia shirika  la  habari  la Ujerumani dpa kuwa  taasisi  hiyo  ya  dunia  imepokea  barua ya Marekani.

Trump  kwa  kawaida  hutumia  hotuba  katika  mikutano  yake  ya kisiasa  kuonesha  mapenzi  yake  kwa  hewa  safi na  maji safi  na salama. "Tuna  hewa  safi  kabisa katika dunia  hapa  Marekani," ni neno  linalojirudia  kila  mara  kutoka  kwa  rais.

Hata  hivyo , uchunguzi  umeonya  kuwa  tangu  mwaka  2016 baadhi ya  aina  ya  uchafuzi  wa  hewa  unaongezeka.

Rais wa zamani wa Marekani Barack Obama akisalimiana na rais wa China Xi Jinping mwanzoni mwa mkutano wa mazingira wa ParisPicha: Reuters/K. Lamarque

Duniani, wanasayansi  kwa  jumla  wana  wasi  wasi  kuwa ongezeko  la  ujoto  unaosababishwa na  utoaji  wa  gesi  chafu  wa binadamu  utasababisha  hali  mbaya  kwa  maisha  katika  sayari hii.

Ufaransa  wakati  huo  huo  imelalamikia  uamuzi  huo  wa  Marekani kuuarifu  rasmi Umoja  wa  mataifa  kuwa  inajitoa  kutoka  mkataba huo wa  paris. Wakati  hatua  hiyo  ilikuwa  ikitarajiwa ,"tunasikitika na  inaufanya  ushirika  wa  Ufaransa  na  China  kuhusu  mazingira na  bio anuai kuwa  muhimu  zaidi", ofisi  ya  rais  wa  Ufaransa amesema  wakati  rais Emmanuel Macron akiwa  katika  ziara  rasmi nchini  China.

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW