1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Marekani: Urusi na Iran zimeongeza uhusiano wao wa kijeshi

10 Desemba 2022

Marekani imesema Urusi na Iran zinashirikiana kwa karibu zaidi kijeshi kuliko hapo awali, kwa Iran kuipatia mifumo ya kisasa ya ulinzi, helikopta, ndege za kivita na ndege zisizo na rubani.

Iran Drone
Picha: SalamPix/abaca/picture alliance

Serikali ya Rais wa Marekani, Joe Biden imeonya kuwa ushirikiano huo wa kijeshi utaleta madhara makubwa kwa Ukraine na majirani wa Iran.

Akiinikuu tathmini ya kijasusi iliyofanywa na Marekani, msemaji wa baraza la usalama la Marekani, John Kirby siku ya Ijumaa alielezea kuhusu kiwango cha msaada wa kijeshi na kiufundi ambao hakijawahi kushuhudiwa ambacho kinabadilisha uhusiano wao kuwa uhusiano kamili wa kiulinzi.

"Marubani wa Iran wanapatiwa mafunzo kwa ajili ya kuziendesha ndege za kivita za Urusi aina ya Sukhoi Su-35, na Iran inatarajiwa kuzipokea ndege hizo katika kipindi cha mwaka ujao," alifafanua Kirby.

Makombora ya Iran ambayo Marekani imedai imeipatia UrusiPicha: Iranian Defence Ministry/AFP

Wakati huo huo, Kirby amesema Iran inafikiria kuanzisha kiwanda cha pamoja cha kuunganisha ndege zisizo na rubani nchini Urusi. Awali Iran ilishutumiwa kwa kuipatia Urusi ndege zisizo na rubani kwa ajili ya kuzitumia katika vita nchini Ukraine.

Kirby amesema usafirishaji wa silaha unakiuka maazimio ya Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa na kwamba Marekani itakuwa inatumia zana ilizonazo katika kufichua na kuharibu mipango na shughuli hizo.

Msaada mpya kwa Ukraine wa dola milioni 275

Siku ya Ijumaa, Kirby alitangaza msaada mpya wa dola milioni 275 kwa ajili ya kuisaidia Ukraine kuimarisha ulinzi wake wa anga, dhidi ya ndege zisizo na rubani za Urusi.

Wizara ya Ulinzi ya Marekani, Pentagon ilitoa maelezo kuhusu msaada huo, ikisema unajumuisha vifaa vya kuzuia mashambulizi ya ndege zisizo na rubani, pamoja na mfumo wa kujikinga na makombora aina ya Himars, maganda ya risasi 80,000, jenereta 150 na vifaa vingine.

Awali, Marekani ilisema kuwa jenereta hizo zinatolewa kwa ajili ya kuisaidia Ukraine na mahitaji ya umeme wakati ambapo mashambulizi ya mara kwa mara ya makombora ya Urusi yanaharibu miundimbinu ya nishati.

Kituo cha kuzalisha umeme cha Ukraine kikiwa kimeshambuliwa kwa makombora ya UrusiPicha: Ed Ram/Getty Images

Msaada wa hivi sasa unafanya jumla ya msaada wa kijeshi uliotolewa na Marekani Kwenda Ukraine tangu Urusi ilipoivamia Ukraine, Februari 24, kufikia zaidi ya dola bilioni 19.3.

Madai hayo yameungwa mkono pia na Waziri wa Mambo ya Nje ya Uingireza, James Cleverly, ambaye ameuelezea ushirikiano wa ulinzi na upelekaji wa silaha kama "mkataba mbaya." Cleverly amesema Iran imekuwa msaada mkubwa wa kijeshi kwa Urusi na uhusiano huo unatishia usalama wa dunia.

Urusi kuipatia Iran msaada wa kiufundi

Amebainisha kuwa Urusi kwa upande wake itatoa msaada wa kijeshi na kiufundi kwa utawala wa Iran, ambao utaongeza hatari kwa washirika wao wa Mashariki ya Kati na usalama wa kimataifa.

Aidha, Balozi wa Uingereza katika Umoja wa Mataifa, Barbara Woodward, ameishutumu Urusi kwa kujaribu kupata silaha zaidi kutoka Iran, ikiwemo mamia ya makombora, na Urusi kuipatia Iran msaada wa kijeshi na kiufundi.

Hata hivyo, Urusi imeikosoa tathmini hiyo ya Marekani, wakati ambapo vita vya Ukraine vikiendelea. Balozi wa Urusi katika Umoja wa mataifa, Vassily Nebenzia amesema madai kuhusu ndege zisizo na rubani kupelekwa Urusi tayari yamekanushwa mara kadhaa.

Picha hii inaonesha kile ambacho Ukraine imeeleza kama mabaki ya ndege isiyo na rubani ya Iran aina ya Shahed, iliyodunguliwa Kupiansk, UkrainePicha: Ukrainian military's Strategic Communications Directorate/AP/picture alliance

"Eneo la viwanda vya kijeshi la Urusi linaweza kufanya kazi vizuri kabisa na halihitaji msaada wa mtu yeyote, kama ambavyo sekta ya kijeshi ya Ukraine kimsingi haipo na inasaidiwa katika masuala ya ulinzi na nchi za Magharibi," Nebenzia aliliambia Ijumaa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Iran imekiri kwamba iliiuzia Urusi ndege zisizo na rubani katika miaka ya nyuma, lakini imekanusha kupelekwa kwa silaha zozote tangu Urusi ilipoivamia Ukraine Februari 24, 2022.

Marekani na juhudi za kutaka Urusi itengwe zaidi

Madai hayo ya Marekani ni sehemu ya juhudi za makusudi za Marekani kutaka kuitenga Urusi na dunia, hasa linapokuja suala la mataifa ya Kiarabu abayo yanaonekana kudhibiti uhasama wa kikanda na Iran na ambayo hayajachukua msimamo mkali dhidi ya uvamizi wa Urusi nchini Ukraine.

Mapema mwaka huu, serikali ya Biden iliishutumu Saudi Arabia kwa kuegemea upande wa Urusi katika mzozo huo baada ya kundi la nchi zinazosafirisha mafuta kwa wingi duniani, pamoja na washirika wao, OPEC+ kupunguza kiwango cha mafuta katika soko la dunia, ili kuongeza bei ya mafuta, ambayo ni muhimu katika kufadhili juhudi za vita vya Urusi

Saudi Arabia na Iran zimekuwa katika pande tofauti katika vita vya miaka mingi vya Yemen.

(AFP, AP)

 

Ruka sehemu inayofuata Taarifa kuu ya DW

Taarifa kuu ya DW

Ruka sehemu inayofuata Taarifa zaidi kutoka DW