Marekani yaeleza wasiwasi kuhusu hali nchini Uganda
11 Septemba 2018Kundi la wabunge akiwemo kiongozi wa upinzania Robert Kyagulanyi, ambaye pia ni mwanamuziki anayejulikana kwa jina lake la jukwaani la Bobi Wine, walikamatwa mjini Arua mwezi Julai. Kyagulanyi, ambaye kwa sasa yuko nchini Marekani anakopatiwa matibabu, na mbunge mwenzake Francis Zaake wanasema waliteswa wakiwa korokoroni.
"Tumepokea ripoti kadhaa za kuaminika kuhusu matumizi ya nguvu iliyokithiri na kamandi ya vikosi maalumu (SFC), zikiwemo za kuwatendea vitendo visivyostahiki wabunge, waandishi habari na watu wengine," alisema afisa wa wizara ya mambo ya nje katika taarifa. "Marekani imebainisha wazi kwa serikali ya Uganda kwamba ukiukaji kama huo wa haki za binadamu haukubaliki."
Rais wa Uganda, Yoweri Museveni, aliyeko madarakani tangu 1986, alionya siku ya Jumapili dhidi ya uingiliaji wa kigeni katika siasa za Uganda. Marekani ni mfadhili mkuu wa jeshi la Uganda, ikilipatia zana za kijeshi, fedha taslimu na mafunzo. Imeipa Uganda silaha, fedha na ujuzi wa kijasusi katika operesheni zake za kumsaka mbabe wa kivita wa kundi la Lord's Resistance Army, LRA, Joseph Kony.
Museveni pia amepokea uungwaji mkono wa kidiplomasia kutoka Washington kutokana na kupeleka majeshi yake katika tume za kulinda amani za kimataifa ikiwa ni pamoja na mapambano dhidi ya makundi ya wapiganaji nchini Somalia.
Wahusika wachukuliwe hatua
Afisa huyo wa wizara ya mambo ya nje alisema ubalozi wa Marekani mjini Kampala haujashirikiana na kamandi ya vikosi maalumu (SFC) tangu mwanzoni mwa 2016 kwa sababu ya wasiwasi juu ya haki za binadamu. Uhusiano wa Marekani na Uganda ulilenga kuimarisha utulivu katika kanda, aliongeza afisa huyo.
"Ni juu ya serikali ya Uganda kuonyesha heshima kwa katiba yake na raia wake na kuendesha uchunguzi wa wazi, wa kuaminika na kwa wakati kuhusu matukio hayo," alisema afisa huyo. "Afisa yeyote wa usalama atakayebainika kutumia nguvu isiyostahili lazima awajibishwe."
Kyagulanyi amepata umaarufu kutokana na mashambulizi yake dhidi ya Museveni. Alishitakiwa kwa uhaini mwezi Agosti kuhusiana na kupigwa mawe kwa msafara wa Museveni mjini Arua. Anakanusha mashitaka hayo na anasema aliteswa wakati alipokuwa korokoroni.
Aliwasili nchini Marekani kwa ajili ya matibabu kutokana na majeraha yake. wawakilishi kutoka wizara ya mambo ya nje ya Marekani walikutana na Kyagulanyi siku ya Alhamisi "kama walivyofanya huko nyuma wakati alipotembelea Marekani," kwa mujibu wa afisa huyo.
Mwandishi: Iddi Ssessanga/rtre
Mhariri: Josephat Charo.