Marekani yaendelea kutathmini hatua dhidi ya Syria
13 Aprili 2018Marekani bado haijafanya uamuzi wa mwisho kuhusu hatua itakayochukua dhidi ya Syria kufuatia madai kwamba ilifanya shambulizi la silaha za sumu. Ikulu ya Marekani imesema hayo baada ya Rais Donald Trump kukutana na washauri wake wakuu wa usalama. Hayo yakijiri Urusi imeionya Marekani dhidi ya hatua yoyote inayoweza kuongeza mvutano zaidi.
Punde baada mkutano wa Rais Trump na washauri wake wa usalama kumalizika, msemaji wa ikulu ya White House Sarah Sanders aliwaambia waandishi wa habari kwamba hakuna uamuzi wa mwisho ambao umeafikiwa. Na kwamba Rais Trump ataendelea kutathmini taarifa za majasusi. Atashauriana na washirika wake wengine; Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Waziri Mkuu wa Uingereza Theresa May, ambao wamesema wataunga mkono hatua zitakazochukuliwa na Marekani dhidi ya Syria. Katika mkutano wao, baraza la usalama la Marekani liliibua hofu ya mgogoro kutanuka zaidi ikiwa hatua za kijeshi zitachukuliwa.
Hofu ya mgogoro kutanuka na raia kuwa hatarini
Waziri wa ulinzi James Mattis ameonekana kuchukua msimamo usiounga mkono matumizi ya nguvu za kijeshi kuiadhibu Syria. Waziri Mattis amesema:
"Kuna wasiwasi kuhusu watu wasiokuwa na hatia na hatutaki kuongeza idadi ya raia waliouwawa. Tutafanya kila tuwezalo kuepuka hilo. Tunajaribu kuepuka mauaji ya raia. Lakini kimkakati, ni vipi tutazuia hali iliyoko isithibitiwe ?"
Maafisa wa nchi za magharibi wanaamini sumu ya chlorine ilitumika katika shambulizi lililofanywa mjini Douma Jumamosi iliopita. Uingereza imetaja idadi ya waliouawa katika shambulizi hilo kuwa watu 75 na kwamba utawala wa Rais Bashar al-Assad unawajibika.
Hofu ya maafisa wa shirika linalodhibiti silaha za sumu kutumika kama ngao
Balozi wa Urusi katika Umoja wa mataifa Vassily Nebenzia, ameonya kuwa kipaumbele nchini Syria ni kuzuia mashambulizi ya Marekani ambayo yanaweza kupelekea makabiliano kati ya mataifa mawili yenye nguvu za kinyuklia ulimwenguni, Marekani na Urusi. Nebenzia ameendelea kusema
"Hatua ya kwanza ni kuwa tunataka mashambulizi yoyote yaepukwe. Lakini bila shaka ni jambo lisilofikirika kuwa Marekani itashambulia kambi yoyote ya kijeshi ya Urusi iliyoko Syria"
Syria imewaalika wachunguzi kutokashirika linalopiga vita matumizi ya silaha za sumu na wanatarajiwa kuwasili nchini humo kuanza uchunguzi kesho. Wanadiplomasia wanahofia kuwa maafisa hao wanaweza kutumiwa kama mateka au ngao katika vita.
Katika tukio jingine, wapiganaji wenye itikadi kali za Kiislamu pamoja na jamaa zao wameondoka katika mji wa Douma. Kundi hilo la Jaish al-Islam pamoja na raia waliondoka usiku wa kuamkia leo kwa mabasi 85 na kuwapeleka katika maeneo ya kaskazini mwa Syria ambayo bado yanadhibitiwa na waasi.
Mwandishi: John Juma
Mhariri: Mohammed Abdul-Rahman